21.7.14

YAJUE MAMBO SABA (7) MUHIMU YA KUTAFAKARI NA KUZINGATIA WAKATI UNAFIKIRIA KUOA/KUOLEWA

Maisha ya ndoa ni maisha ya kipindi cha mwisho kwa Mwanadamu kilicho na mitihani mingi sana, kwani ni darasa tosha kwa wanandoa, na ndiyo maana katika uchumba unatakiwa upitie misukusuko kwani ni mojawapo ya mitihani ili ufikie kupata cheti wakati wa ndoa, na nikatafakari sana kwamba hapa duniani mwanadamu anapata cheti baada ya kufaulu mitihani, lakini kwa ndoa nikashangaa mtu anapewa cheti kwanza ndipo anapoingia kwenye mtihani wa maisha ya ndoa, sasa ni wewe kufaulu au kushindwa! Hivyo ili kuweza kuishi maisha ya ndoa yaliyo mazuri na yenye furaha ni vyema katika uchumba ukajua namna ya kujibu maswali kwenye mtihani ulio nao (Uchumba kama mtihani, na cheti ndicho kinachowakilisha kufaulu kwako na ndipo unaingia kwenye maisha ya ndoa, Haleluya!!) 

  1. Tambua unapoamua kuoa au kuolewa unakuwa unaunganisha familia tatu tofauti na zenye maagano tofauti.
Familia ya kwanza ni yenu nyie wawili yaani mke na mume, siyo rahisi kuweza kuishi kiraisi na mtu ambaye amelelewa kwao na mazingira tofauti na ya kwako, malezi tafauti kabisa, mawazo na mtazamo ni tafauti, mara ghafla mnaanza kuishi pamoja, na mnatakiwa kuwekana wazi kwa kila jambo na kufanya maamuzi yasiyoweza kuwafanya mgombane. Sasa katika nyie wawili mtegemee kujenga na kuzaa familia yenye mtazamo na taswira tofauti na familia zenu mlikotoka. Na familia zinazokuja hizi mbili ni upande wa mwanamke na upande wa mwanamume na kila familia ina tabia zake.
         Familia zingine badala ya baba kuwa kiongozi wa nyumba, utakuta mama ndiye kiongozi wa nyumba, inamaana kila analosema mama pale nyumbani ndilo linafwatwa, wala baba hawezi kuwa na maamuzi yoyote yale juu ya uamuzi atakaoufanya mama, sasa chukulia ndiyo unaoa msichana kwenye hiyo familia na ghafla anaanza kukuendesha na kuwa na sauti ndani ya nyumba kwa kila kitu, na kwa sababu alikotoka kwenye familia yao ameona mama ndiye kiongozi na mwenye sauti ya mwisho wa familia, na kwa sababu wewe mwanamume hayo mambo kwako ni mageni basi lazima muingie kwenye ugomvi.
         Umewahi kufikiri unaenda kuo/kuolewa kwenye familia ambayo ni wachawi! Vijana wengi kwa sababu ya tamaa zao wamejikuta wameishia kuoa/kuolewa na watu wachawi. Kuna kijana mmoja alikuwa ni mtumishi mzuri sana na Mungu alikuwa anamtumia vizuri sana lakini ilipofika kipindi cha kuoa akaaamua kuchagua binti fulani kanisani humohumo na huyo binti alikuwa anaonekana yupo safi kiroho na alikuwa mzuri hata wa sura, lakini watu walimshauri kwamba huyo binti hakufai na kwa huduma uliyonayo kwa kweli itakufa. Yule mtumishi hakuweza kuelewa ushauri wa wale watu, alin’gan’gana mpaka akamwoa yule binti na ilipofika kipindi wanapokuwa kwenye huduma vijijini pamoja na watumishi wengine, yule mtumishi akawa anashindwa kutumika kama hapo awali, mara Mungu akamfunulia mtumishi mwenzake, usiku akamwona yule mtumishi anakabwa na mke wake mpaka anaelekea kufa, ndipo wakatambua kwamba yule binti alikuwa siyo mzuri yaani alikuwa mchawi, basi mpaka sasa yule mtumishi anaishia kuwa kama waumini wengine kanisani kwani huduma ndiyo imekwisha kabisa mpaka sasa.
        Familia zingine huwa ni wachafu sana, yaani siku ukaenda nyumbani kwao ghafla bila taarifa, utashanga takataka mpaka mlangoni na mara nyingine hata kupiga deki ndani ni shida tupu, sasa unajiuliza humu ndani naingia nivue viatu au? Maana nikivua ni lazima nitachafuka na nisipovua watasema hana adabu. Sasa umewahi kufikiria ndiyo mwanamke anakuja unamwoa utashaagaa hata kitanda kutandika ni shida, nguo zinakaa mpaka sebuleni. na wanaume, siku mke kasafiri utajua tu kwamba leo mke wa fulani kasafiri, utashangaa kuona sebuleni pako ovyo, vitambaa ni balaa tupu utasema kunawatoto walikuwa wanacheza na kama alikuwa anajipikia basi utavikuta vyombo vimejazana na vinazungukwa na nzi, sufuria zina masizi mpaka ndani sasa sijui yaliingiaje mi sijui! Ni aibu hiyo jamani!, sasa hali ikiwa kama hivyo itapelekea magonjwa yasiyoeleweka. Badala ya kuona raha ya ndoa sasa unaanza kuona karaha ya ndoa kisa hukufanya uchunguzi na kufikiria kabla hujafanya maamuzi.
       Watu wengine ni wavivu sana, maandiko yasema “asiyefanya kazi na asile”, kunafamilia zingine jamani ni tabu tupu, ukiangalia wanapenda kuvaa vizuri sana na kujipenda sana na kanisani wanaenda sana, lakini ukiuliza wapi wanashamba la kulima watakwambia hamna. Kweli wengine wanaishi mjini mashamba ambapo hamna lakini nina maana hata sehemu ya kujipatia riziki angalau kidogo, wengine hata kujishughulisha na shughuli ndogondogo tu huwa hawawezi, hasa vijana wa kiume utashanga kuanzia asubuhi mpka jioni anaangalia Vidio (Television Vidio (TV)) na hapo anamchumba na anapanga kuoa, hata godoro hana na bado anakaa kwa wazazi wake, yeye huwa anasubiri asubuhi ifike anywe chai aliyopika mama au dada ndipo aende kijiweni na ikifika mchana atarudi kula chakula cha mchana na kurudi tena kijiweni, hivyohivyo na jioni na kama ndiyo siku ya ibada ndipo ataoga na kuomba sadaka kwa mzazi halafu aende kanisani. Mhh Mungu atusaidie sana.
       Familia zingine zinamazindiko sana, kwamba kila atakaye mwoa huyu binti wa kwanza ni lazima afe, au wanamwapisha kwamba huyu binti atakuwa anaishia kuwa mjane, pia hata upande wa mwanamume huwa mazindiko yapo, kwamba huyu kijana kila akioa hatakuwa anapata watoto. Nilipigiwa simu siku moja na binti, akaniambia nimwombee kwani alinenewa na shangazi yake ya kwamba hatakuja kupata mume wala mafanikio yoyote katika maisha yake yote, na hapo alipo alikuwa amewahi chumbiwa mara tatu na anaishia kuachwa pasipo na sababu, na sasa anaishia tu kukaka kwa dada yake, usije kushangaa hata mwenyewe unajaribu kupanga kuoa/kuolewa kumbe umefungwa lakini yote ni ushirikina wa kifamilia au huo ukoo.
       Pia kuna familia zingine au makabila mengine huwa wanadai mtoto wa kwanza kuzaliwa ili atolewe kama kafara, na usipoelewa hili litakugharimu pindi tu utakapokuja kumpoteza huyo mtoto na ndipo utakapoelewa, na ndiyo maana tunasema kijana kaa vizuri na Mungu naye atakupa macho ya rohoni utaona wapi panafaa kuoa/kuolewa. Kumbuka pia magonjwa mengine ya kurithi huwa yanafwatilia watoto wa kwanza kama vile kuugua kichaa, kifafa, kifua kikuu, UKIMWI n.k na hizo zinakuwa ni roho tu zinazofuatilia familia. Kumbuka unapounganisha mambo yote ya familia ya upande huu na upande mwingine unategemea utapata nini hapo?

  1. Unapoamua kuoa/kuolewa utambue unaenda kuwajibika zaidi
Kumbuka ya kwamba unapoamua kuoa/kuolewa unaenda kuanza maisha ya kipekee kwani hiyo ndiyo ngazi ya maisha yako ya mwisho mpaka kufa kwako, kumbuka siku utaitwa baba/mama mpaka utakuja itwa bibi/babu, kama Mungu atakujalia maisha marefu, hivyo kumbuka utakuwa umekusanya ndugu wa pande mbili zote, sasa usije sema mi naweza nikamlea mke wangu tu! Hapana, kumbuka kuna ndugu wa upande wa mke/mume wako watahitaji msaada je utaweza kumudu? Na maandiko yanasema;
“Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini” (1Timotheo 5:8)
Ni aibu na ni dhambi, pale unaposhindwa kuwahudumia ndugu zako wa nyumbani mwako, kumbuka kunamaradhi, kuna misiba, kuna wengine wanasoma kama mdogo mtu au kaka mtu hao watahitaji matumizi ya shule au ada, kuna mambo ambayo ulipokuwa peke yako uliona ni rahisi kufanya lakini pindi unapokuwa na ndoa unatakiwa kuwajibika zaidi.
       Mara nyingine kwa kijana wa kiume unaoa msichana ambaye ni wa kwanza kwao au ni tegemeo kwenye familia yao, na pindi unapoamua kumwoa inamaana tegemeo lote linakuwa ni wewe, sasa sikwambii usimwoe! Hapana, baali hakikisha umejipanga vizuri kukabiliana na majukumu aliyokuwa nayo kwao kwani huwezi kuwatupa ndugu wa upande wake, na siku nyingine watapenda kuja kukutembelea kwako, na wengine watapenda kulala kama ni mbali kidogo, sasa itategemea umejenga nyumba au umepanga nyumba ya namna gani, nasema hivi kwani nimeona pindi tu wanandoa wanapoingia wakiwa hawana hata muda mrefu huwa inaanza misuguano na ukifwatilia utakuta ni ndugu wanajaa nyumbani. Sasa jiandae unaeingia kwenye ndoa kubeba ugeni na kuwajibika kwa hali na maali.
        Kumbuka kunakuwajibika kimawazo pia, muda mwingine kunakuwepo na vikao mbalimbali vya familia ya upande wa mwenzi wako, nawe kama mwanafamilia unatakiwa kuwa na upeo wa kuweza kuchangia hoja na mawazo ya kimsingi, utashangaa shemeji mtu kwenye kikao anakuja ananuka pombe na anayoyafanya pale kwenye kikao mwenyewe mwenzi wake utatamani uzimie. Sasa kama yeye mwenyewe anashindwa kujilekebisha ataweza kweli kumpa mtu mawazo ya kumjenga? Na ndiyo hao wanafika kipindi wanatembea na wafanya kazi wao wa ndani na inayopelekea mpaka ndoa kuyumba.
        Hasa kwa mabinti nataka mnisikilize, ni aibu sana binti unaeingia kwenye ndoa halafu hujui kupika, unapika wali jinsi unavyoukologa loh! Utazani unakologa uji, na ukipika ugali unaekula utatakiwa uwe na maji ya moto pembeni kwani lazima ukutane na mabonge ya unga katikati ya ugali, sasa ni aibu na ndiyo maana wanaume wanaamua kula huko nje ndipo wanarudi nyumbani. Pia wanaume nanyi mnashangaza sana wengine hata kusonga ugali ni shida sana, na pindi mke anumwa wewe unaamua kununua chipsi, sasa sijui mtakulahizo chipsi mpaka lini, siku umeingia jikoni unaipua ugali mbichi kabisa. Nakumbuka nilitembelewa na rafiki yangu mmoja na mimi nilikuwa sishindi nyumbani, na pale nyumbani kuna kila kitu cha kuweza kupika, siku nimetoka kazini narudi nyumbani nikakuta hajapika kitu, nilipomuuliza mbona hujapika? Na umekula nini? Akasema nilinunua chipsi, nami nikajua aliamu tu kununua chipsi pengine kwa sababu ya uchovu, sasa kesho yake nikamwabia twende sokoni ukaje na mboga kwani mimi sitarudi! Tulipofika sokoni nikanunu mboga na nilipomwambia aendelee kupika, akasema utakuja kupika mwenyewe kwani mimi sijui kupika! hah! Yaani nilishikwa na butwaa, na nikweli kabisa alikuwa hajui na alikuwa kijana amemaliza chuo kikuu.
       Sasa unielewe kwamba unapooa unaenda kuwa na mipaka, kwamba ni lazima ukawajibike tu na hiyo mipaka ni ya baadhi ya mambo mengine kutokuyafanya, kama vile kurudi usiku nyumbani, kama ulikuwa unakesha kuangalia mpira kwa jirani yako sasa itabidi hiyo tabia ife, kwani siku utarudi utakuta mwana si wako.
        Kama bado hujaoa, weka mpangilio ni lini unaoa kusudi upangilie mipango na namna gani utaweza kukabiriana na majukumu, shida ipo sana kwa vijana wakiona fulani kaoa basi utashangaa naye huyu anakimbilia kuoa, we unajua mwenzio alivyojipanga? Weka malengo ndani ya muda fulani utakuwa umefanya mambo kadhaa ndipo uingine kwenye ndoa.
“Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”
 (Mhubiri 3:1)
Ujue kila kipindi unachopitia kuna takiwa uchukue hatua za mabadiliko kutegemeana na majira, na kama unajipanga kuoa baada ya miaka miwili inamaana kunamambo utatakiwa kuyafanya hapa katikati ili kujiandaa kukabiriana na majukumu ya ndoa. Pia kwa kadri tathmini utakavyokuwa unaiona ni rahisi kuwa na taswira nzima ya ndoa yako na kujua watoto utakao kuja kuzaa. Kunawengine wanaingia kwenye ndoa hata hawaelewi watazaa watoto wangapi na wengine hata wakati wa uchumba huwa hawajadili kwamba waje wazae watoto wangapi, sasa inapotokea mmeingia tayari kwenye ndoa na mwenzio anataka watoto sita na wewe unataka wawili sasa sijui mtakata rufaa wapi, mimi sijui! Zaidi mtakuwa mnaleta kuvutana kwenye suala la idadi ya watoto kila siku.
        Unapoamu kuoa angalia kwanza wewe ni tegemeo kwenye familia au lah! Unawadogo zako wanatakiwa kwenda shule na bado hawajaenda au ndiyo wapo shule, elewa unapoingia kuoa kabla ya hao watoto kuwawekea msingi mzuri ukitegemea kwamba ukioa utawasomesha, uwe na uhakika kabisa watayumba kwani maamuzi yako ya kuwasomesha ukiwa kwenye ndoa ni lazima umshirikishe mke wako, na siyo rahisi kukubali kila mwisho wa mwezi mshahara uende nyumbani kusaidia ada ya wadogo zako, na mara nyingi familia zimekwama kielimu na maendeleo mengine kwa sababu tu kaka aliyekuwa mwenye uwezo kaoa na baada ya kuoa akasahau kusaidia wazazi na wadogo zake.


INAENDELEA

iii. Unapoamua kuoa/kuolewa kuna baadhi ya marafiki utajikuta mnatengana au mnaungana.
Ukisoma (Hesabu 12:1-2)
“Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi, wakasema, Je! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao
Ukiendelea kusoma mistari huko mbele, utaona Mungu anaingilia kati na hatimaye Miriamu anapigwa na Mungu kwa pigo la ukoma kwa sababu waliingilia ndoa ya Musa kwa kumsema vibaya mtumishi wa Mungu. Ni muhimu sana kabla ya kuanza kuwashirikisha watu juu ya mchumba amabye pengine Mungu kakuonesha, sasa unahitaji uthibitishe angalau kwa watumishi wenzako nao waombe waone kama ni mpango wa Mungu au la!, sasa umewahi kufikiri Musa angewashirikisha hao ndugu zake kabla hajaoa! ni lazima wangempinga tu!
       Ni muhimu sana uelewe mapema kwa kuchunguza marafiki wa mtu utakaeoana naye, kusudi baadaye isije ikaleta shida kwenye ndoa, kuna baadhi ya marafiki hawawezi kukushauri uoane na fulani pengine ya chuki zao binafsi, sasa itakapofikia baadaye mmeoana tayari tambua hawataweza kuendelea kujenga tena urafiki na ninyi, hivyo itapelekea chuki isiyokuwa na maana. Kikubwa ni kuchunga sana marafiki wanaokushauri juu ya mtu wa kuoa, je! kunauhusiano gani na huyo unaetaka kuoana naye?
      Wajue mapema marafiki wa mchumba wako mapema, na kama ni wazuri itabidi uendelee kumshauri awe nao lakini kama umechunguza ukaona wanakasoro itabidi uingine kwenye maombi Mungu akuongoze namna gani umshauri ili aweze kuachana nao. nimeona kuna marafiki ambao wanakuwa ni kero baada ya mtu kuoa na wengine wanadiriki kuwataka kimapenzi wake za rafiki zao, hiki kitu ni cha kukiangalia vizuri na hasa kwa marafiki wengine ambao ni walevi na wavuta sigara, inapofikia mchumba wako amebadilika kama alikuwa na hizo tabia kabla ya uchumba na akawa bado anao hao marafiki uwe na uhakika pindi mtakapooana atashawishika kurudi kwenye zile tabia za zamani kama marafiki zake.
      Na mara nyingi sana nimeona watu wakiwa wanawashirikisha marafiki zao sehemu ya kuo/kuolewa huwa haohao marafiki zao wanawageuka na kuanza kufanya mahusiano wao. Ukiona sehemu kunakiota cha ndege usije ukaenda kuomba msaada namna gani ya kumla kabla hujamkamata utaishia kusema ilitakiwa iwe mimi!
      Kumbuka namna ya kujinasua kwenye huo mtego, utashanga hadi unahama mji, na ndiyo maana watu wakioa tu, wanaamua kuhama miji ya kuishi, na ni muhimu sana ili kuondoa mazingira yale ya zamani ambayo yangeweza kukuwekea vikwazo kwa baadhi ya watu jinsi walivyokuzoea, kwa mfano kama ulipanga nyumba, utambue kuna majirani wataendelea kuja na pengine walizoea kuangalia Vidio (TV) ndani kwako mpaka usiku, kitu kitakachopelekea kumkwaza hata mke wako. Sasa inapotokea umeoa ni bora uhame na itabidi mkubaliane sehemu ya kuishi baada tu ya ndoa kusudi msije mkapishana kwa ajili ya mazingira ya kuishi, wengine wanaamua kwenda mkoa kwa mkoa sasa kama mke anataka Mwanza na mume anataka Mbeya, si ndiyo chanzo cha kuvunjika kwa ndoa, kumbe ni bora mkubaliane mapema kabla ya ndoa ili mmoja wenu akigoma kuhama kutokana na sababu zake binafsi muwe tayari kutokuoana. Lakini wengine hawataki kuhama kutoka Buguruni kwenda Ubungo ila yeye anataka Gongolamboto sasa ni bora makubaliano mapema, kwani muda mwingine anakataa kuhamia huko kumbe wakati bado hamjaoana aliwahi kuolewa huko na akaachika, pengine amewahi kufumaniwa mazingira hayo, si unajua ndoa za siku hizi vijana wanaonana kwenye daladala tayari wanapendana na kesho wanatangaza harusi bila hata kumchunguza vizuri mwenzake.

iv. kuoa au kuolewa kunaweza kukakubadilisha  utumishi wako.
“Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakaugeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake”
(1Wafalme 11:4)
         Ukisoma mstari wa 3 utaona idadi ya wake aliokuwa nao Sulemani, alikuwa na wake mia saba na masuria mia tatu yaani wake wa nje ambao wanajulikana kwamba anatembea nao, na wote hao wake walikuja siyo kwa sababu ya uzuri wa sura yake, maana maandiko hayajasema lakini kutokana na maandiko inaonesha ni kwa sababu ya utumishi aliokuwa nao pamoja na hekima aliyokuwa nayo, hivyo unapokuwa mtumishi angalia hata watu wanaotaka ushauri kutoka kwako wasije wakawa wanataka kuteka utumishi wako. Sulemani na hekima yote ile ambayo aliambiwa na Mungu kwamba hayupo na hatakuja kutokea Mfalme kama wewe na hatima yake anaishia vibaya na utumishi wake.
“Samsoni akaenda Gaza, akaona huko Mwanamke kahaba, akaingia kwake……….Wafilisti wakamkamata wakamn’goa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza”
(Waamuzi 16:1;21)
Najua unamkumbuka Samsoni ambaye alikuwa amemwoa Delila, Delila aliingia kwenye ile ndoa akiwa na jambo moja tu! Na lilikuwa ni namna gani ya kuharibu kusudi la Mungu ndani ya Samsoni, Shetani anawinda sana kusudi la Mungu ndani ya mtu hasa anaye jua kabisa kwamba atakuwa ni Lango la Familia, Nchi, n.k na atahakikisha anatumia mke utakayemwoa kusudi akubane, wapo watumishi wamekwama kihuduma kwa sababu ya vikwazo vywa wake zao. Kuna dada fulani alikuwa safi sana kiroho lakini akaja akaolewa, ghafla kanisani akaachishwa kwenda na mume wake.
        Mara nyingi Mungu huwa anaachilia kusudi (hasa huduma) kwa mwanamume, pia kwa mwanamume huwa linajidhihirisha kwa urahisi na huwa ni wepesi kutambua wito wao lakini mwanamke zile hisia za kudhihirisha huwa zinakuwa mbali, na ndiyo maana utashangaa utumishi unachanua baada ya kuolewa tu! na tena kaolewa na mtumishi ndipo utatambua. Sasa Shetani anachofanya kwa mwanamume huwa anakusogezea Delila au Mke wa Ayubu kusudi aharibu kile Mungu anachotaka kichanue.
       Inavyoonesha Delila alikuwa ni mzuri sana wa umbile la nje na sura, na ndiyo maana alikuwa kahaba (anajiuza), na siku hizi vijana wanaangalia sura na umbile la mwanamke na ajabu yake wanabeba akina Delila hatimaye ndoa zinaishia robo ya safari, nataka nikwambie mke siyo sura nzuri wala umbile zuri, baali ni moyo wake. Nakumbuka kuna rafiki yangu tulipita mahali fulani halafu ghafla tukakutana na rafiki yake huyo rafiki yangu, na yule rafiki yake alikuwa na mke lakini kwa mwonekano wake alikuwa hawaendani, ninamaana mwanamume alikuwa kidogo anamwonekano mzuri (Handsome) kuliko mke wake. Sasa yule rafiki yangu akaniambia “huyu jamaa utazani alichagua mke akiwa amesinzia?” “nikamwambia jipange tena kuongea maneno hayo” na yeye alikuwa bado hajaoa, nikamwambia usitukane mamba kabla hujavuka mto, siku ukijakumwomba Mungu akupe mke akakuletea asiyekuwa na pua sijui utasemaje! Na huwezi kukata rufaa ya maombi.
“Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa” (Mithali 31:30)
      Mwanamke anaweza akawa mzuri sana lakini akawa kikwazo kikubwa kwenye ndoa yako, utumishi wako/katika mahusiano yako na Mungu, pia huyohuyo mwanamke anaweza akawa ni nguzo nzuri kwenye huduma yako inategemeana umesugua goti kwa namna gani kumwomba Mungu akupe atakaekufaa.


v. Kuoa/kuolewa kunakutenganisha na wazazi wako.
“Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja”
 (Mwanzo 2:24)
Watu wengi nimeona hasa wasichana wanapokuwa wametoka kuolewa tu! anaanza kupungua mwili, na siyo kwamba hali chakula, bali anakuwa na mawazo na kutokusahau nyumbani, kama hauna msuli wa kusahau wazazi nakwambia usiwe na halaka ya kuolewa subiri kwanza uondoke umekomaa, na hii huwa inaathiri sana wanadoa kwani mwanamume hawezi kumtamani mke wake vile inavyotakiwa, yaani ataonekana kama anamlazimisha hasa pindi wanapoingia faragha ya ndoa, inafika hata wakati wa kula chakula huwa inakuwa ni ngumu kidogo kwa mtu ambaye bado hajasahau nyumbani.
        Unapokuwa unaambatana na mkeo/mumeo inamaana mnakuwa na nia moja, dhumuni moja ili kufikia malengo katika ndoa yenu na pindi matatizo yanapotokea ni rahisi kuyamaliza nyie wenyewe, kunatatizo moja ambalo linasumbua sana ndoa changa, ni pindi tu wanapokorofishana tena sababu yenyewe ni ndogo sana ambayo mnaweza kuitatua nyie wenyewe kwa kukaa chini, utashangaa mwanamke anatoa taarifa nyumbani mara moja, na siku hizi kuna Simu, hivyo atapiga Simu kwa ndugu zake wote na kama wanaishi karibu na nyumbani uwe na uhakika ataenda nyumbani ama ndugu zake watakuja ilimradi wapate taarifa vizuri, lakini madhara yake ni makubwa sana kwani utakuja kujutia mwenyewe hapo baadaye. Ujue watatokea washauri ambao watakushauri vibaya juu ya ndoa yako, pili watatambua madhaifu yenu katika ndoa kitu amabacho siyo vizuri.
         Nilikuwa mkoa fulani sitaki kuutaja, nikawa kwenye huduma na mara nikaitwa na dada mmoja aliyekuwa ni mtumishi mwenzangu ili nimsikilize yule kaka aliyekuwa amekaa naye, na shida yake yule kaka, nilipomsikiliza alisema hivi, alikuwa na mke na huyo mke alimkimbia kwa sababu ya ugonjwa wa mwanamume na huo ugonjwa ni kwamba alikuwa anakojoa kitandani na alisema ukweli yule kaka, lakini nilipoendelea kuhojiana naye nikatambua kwamba yule mke alishawishiwa na wazazi wake, na kwa sababu aliwashirikisha wazazi wake jambo la mume wake ndiyo mana wakamshauri amwache. Lakini Mungu ni mwema yule kaka tukamwombea na akafunguliwa na ile hali ya kukojoa ikaisha na baada ya muda akapiga simu kwamba amepata mchumba mwingine.
         Unapoambatana na mkeo na kuwaacha wazazi wako mnatakiwa kushirikishana nyie wenyewe kwa kila kitu, usije kumficha jambo mwenzi wako. Kuna ndoa fulani ni mpya tu na niwapendwa katika Kristo lakini mwanamume hataki kabisa kumshirikisha mke wake, hata juu ya mshahara anaoupata hataki kumwambia mke wake, ila kanisani anaweza akapeleka sadaka hadi Laki tano, na yeye kwake ni kawaida na huwa wanaingia mpaka kwenye ugomvi na mke wake kwa kupigana kabisa tena wanapelekana mpaka hospitalini, sasa unategemea kunabaraka zitakuja kweli hapo, angalia Petro anavyosema;
Kadhalika ninyi waume kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusikilizwe” (1Petro 3:7)
Uwe na uhakika ndoa isipokuwa na amani, baraka zinazoingia hapo zinakuwa ni butu, sasa kama moyo wako utaendelea kuambatana na wazazi ukiwa bado uko ndani ya ndoa yako ujue hamtaweza kuelewana na mke/mume wako kwa sababu hamtakuwa na nia moja, kila mtakaloshauriana hamtaafikiana kwa sababu ukifikilia hilo jambo likitendeka utahamishwa pengine kikazi na itakupelekea kwenda mbali na wazazi. Nakumbuka kaka mmoja alinifuata akaniambia shida yake halafu nikamuuliza mke wako yuko wapi? Akaniambia alikataa kuhama pamoja na mimi kwa sababu mama yake huwa anamsaidia kazi ndogondogo pale kijijini. Sasa inamaana huyu mwanamke hajatimiza neno “kuambatana”.
          Suala la mzazi anapokuja kuwatembelea nyumbani na kumbadilisha kuwa ni mwanamke wa kazi hiyo siyo tabia nzuri, kunandoa moja haikuwa na mahusiano mazuri kati ya mke na mume, ikafika mama wa mwanamume akawa yupo pale nyumbani kwa kitambo kidogo, cha ajabu nikwamba yule baba alikuwa anampatia mama yake mzazi pesa za mahitaji ya pale nyumabani kama ni sokoni na kila kitu, yaani yule mama ndiye aliyekuwa ni mpangaji wa kwamba leo mtakula hiki au hiki, sasa mke mwenye nyumba hakuwa na sauti jambo ambalo likapelekea mpaka kutengana mpaka sasa. Jihadhari sana kijana uliye kwenye ndoa na wewe unaetaka kuingia kwenye ndoa.


Itaendelea...............

+255 (0) 712 201 073/ +255 (0) 752 005 418

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni