NAMNA YA KUKUSAIDIA KUOMBA VIZURI NA KWA MUDA MREFU




  1. TAFUTA MAHALI PAZURI PENYE UTULIVU. (Marko 1:35)
Ili uweze kuomba kwa utulivu na kwa umakini, chagua au tafuta mahali pazuri patakapokupa utulivu katika kuomba (Concentration in prayer). Ndio maana Mungu alipenda kuongea na Musa mlimani, (Kutoka 24:12-18). Hata Yesu alizoea kwenda kuombea mlimani, mahali palipo mbali na vurugu za watu, alipenda kwenda mlimani, (Mathayo 14:22-23). Tafuta mahali patulivu; chumbani, kanisani, mlimani, n.k (Mt 6:5-6).
     Mazingira yakiwa na kelele, htaweza kuomba kwa umakini, na hata usikivu wa kumwelewa Mungu hata akisema nawe huwa inakuwa ni ngumu sana.

  1. TENGA MUDA MZURI (Mhubiri 3:1-7)
Ukitaka uombe kwa umakini mzuri na kwa mzigo, chagua muda mzuri ambao utakuwa unahakikisha akili yako na mwili wako viko freshi. Usije ukalazimisha kuomba hata kama akili yako au mwili wako umechoka sana. Kila jambo lina wakati wake. Kama umechoka sana, huo si muda wa kuomba, bali ni wa kupumzika. Usilazimishe ratiba. Ni bora upumzike ili baadaye uweze kuomba vizuri. Usije ukajikuta unapiga tu miayo na hujui unaomba nini. Penda kuomba wakati unanguvu ya akili a mwili, ili uwe makini kuongea na Mungu kwa akili timamu. Ndio maana Yesu alipenda kuamka alfajiri sana kwenda kuomba mlimani.
       Hata nyumbani, jaribu kutenga muda wa kuangalia TV, na siyo muda wote unatazama TV mpaka inakuondolea mawazo ya kuomba. Mimi huwa nina muda maalumu wa kutazama, ni tarifa ya habari saa 2 usiku mpaka saa 3:30 ndipo ninazima, na ninaenelea na ratiba zingine. Nidhamu ya kumtafuta Mungu kwa kumtengea muda wa kuongea naye ni vizuri zaidi kwani itakutengenezea heshima mbele zake. Biblia inasema ”nawapanda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii watanina” Mith 8:17. ukimheshimu Mungu kwa kutenga muda kwa ajili yake, na yeye atakuheshimu.

  1. OMBA KATIKA ROHO (Nena kwa Lugha). (Rum:26-27, Waefeso 6:18)
Kuomba kwa Roho, yaani kunena kwa Lugha, kunamfanya Roho Mtakatifu anayejua kuchunguza mioyo yetu na haja tulizonazo, anakamata ulimi wako kuhakikisha anakuombea vile Mungu atakavyo, na kwa kutegemeana na mzigo ulionao mpaka uishe ndani yako ndipo anakuachia. Hivyo kwasababu mahitaji tunayomengi, huwa unaweza ukajikuta unaomba kwa muda mrefu zaidi mpaka Mungu aone mpenyo wa kuachilia ukiombacho. Tunapoomba kwa akili za kibinadamu, mungu anasikia pia, lakini maombi yako yanakuwa na mipaka, kwa sababu akili yta mtu haijui kila kitu. Bali Roho wa Mungu anajua kila kitu. Naye hutupa kipawa cha kuomba kwa lugha ya mbinguni iliyo bora zaidi. (Yuda 1:20, Marko 16:17, 1Kor 14:1-4, 15-16,7)

  1. WAKATI MWINGINE OMBA KWA KUFUNGA (Mathayo 6:16-18)
Kufunga kunasaidia kudhoofisha mwili, ili roho iwe makini zaidi kuongea na Mungu kwa kina zaidi. Mwili huu siku zote haupendi kufanya mambo ya Mungu. Unapofunga, unajionesha mbele za Mungu kujitoa kwako kama dhabihu iliyo hai. Unampa Mungu kipau mbele kuliko vyote, ni badala ya kutoa sadaka ya pesa au ya aina yoyote, kwani kule kuomba tu ni sadaka tosha mbele za Mungu (Mith 15:8). Kama Yesu alivyojitoa kuwa dhabihu takatifu kwa Mungu kwa ajili ya mwanadamu, ndivyo vivyo hivyo, unapofunga unajitolea kwa ajili yako na kwa niaba ya wengine, (Isaya 58).
      Mara nyingine, kama unapenda kufanya ibada jioni, pengine majira ya saa 2 usiku, kwa watu wengi muda huo unakuwa ni muda wa chakula cha jioni. Lakini nataka nikwambie kamba, mtu akisha shiba huwa mwili unachoka na kupelekea kulala (unalewa). Kwenye chakula kunamchanganyiko wa vitu vingi ambavyo vipo kwenye chumvi ama sukari. Mfano ukinywa chai ni lazima usikie kulala tu! Kwani kuna sulpher ambayo inapelekea kulewa kwa akili na mwili. Ndiyo maana ukishiba tu, unasikia kulala.
      Mara nyingi mimi napenda kula mchana vizuri, halafu usiku au jioni, huwa napenda kutumia matunda na vitu laini visivyokuwa na mchanganyiko wowote. Huwa siwezi kusikia uchovu kama vile ningekula chakula cha kawaida.

  1. MARA NYINGINE OMBA NA RAFKI YAKO. (Mhubiri 4:9-10)
Biblia inasema ”Ni heri wawili kuliko mmoja”. Kuna faida ya kuomba pamoja na rafiki yako. Kwanza, mnapokuwa wawili au watatu, inaleta hamasa na ari ya kuomba zaidi. Si rahisi kujisikia mvivu unapokuwa na waombaji wenzako. Pili; nguvu ya kiroho inaongezeka. Neno linasema, mwombaji mmoja anafukuza adui elfu moja, bali wakiwa wawili, wanafukuza elfu kumi, (siyo elfu mbili! Ni elfu kumi!, (Kumb 32:30). Hiyo ni kanuni ya mbinguni/Ki-Mungu. Kadri mnavyoongezeka, ndivyo na nguvu ya Mungu inaongezeka.
       Hivyo, wakati mwingine omba na rafiki yako unayemwamini, unayeweza kumshirikisha mambo yako ya binafsi. Mashujaa wengi wa imani, walikuwa na marafiki zao wa kiroho. Mfano:- Mathayo 17:1-9.
§         Musa – alikuwa na Joshua, Haruni na Huri.
§         Eliya – alikuwa na Elisha
§         Elisha – akaja akawa na Gehazi
§         Daniel – alikuwa na Shadrack, Meshack na Abednego.
§         Yesu – alikuwa na Petro, Yakobo na Yohana.
§         Paulo – alikuwa na Barnaba, Timotheo na Tito.

Kama huna rafiki wa karibu wa kuomba naye, usikurupuke kujichagulia. Tulia umwombe Mungu akupe mtu atakayekuwa wa msaada kwako. Mtu mtakayefungamanishwa naye katika roho, hata kama mko mbali mbali kijiografia, lakini katika roho mko na umoja mzuri wa imani. (Mathayo 18:18-19)

  1. ITAMBUE MIKAO  INAYOKUPA UHURU NA UPAKO UNAPOOMBA.
Kila mtu ana namna yake alivyozoea akiwa anaomba, lakini kunamikao mingine ambayo ukajifunza/ukaiiga, inakupa upako, kutegemeana na uelewa wa huo mkao unamaanisha nini mbele za Mungu. Katika kuomba kwa muda mrefu, mkao uliouzoea utakusaidia kwenda mwendo mrfu. Yakupasa kujua nguvu yako na udhaifu wako. Wakati wa kuomba, epuka mikao inayokuchosha haraka na tumia miako inayokupa nguvu zaidi. Kwa mfano, ukiwa umechoka usipende kuomba kwa kupiga magoti au kuegemea kitandani. Ni bora uombe ukiwa umesimama au unatembea tembea, ili kuepusha usingizi na uchovu. Waliozoea maombi wengine huwa wanabadilisha badilisha mikao ili isiwachoshe.
         Mifano ya waombaji walioomba kwa mikao tofauti na kwa sababu za Ki-Mungu.
    • Mzee Ibrahimu: aliomba kwa kusimama, (Mwanzo 18:22)
- Kusimama, maana yake kuutambua wajibu wako, kwenye eneo lako, muda wako maalumu, na kile unachotakiwa kusimamia. (Habakuk 2:1)
    • Daniel: aliomba kwa kupiga magoti. (Dan 6:10)
    • Mtume Paulo: aliomba kwa kupiga magoti (Efeso 3:14)
    • Bwana Yesu: aliomba kwa kupiga magoti. (Luka 22:41)
Nguvu iliyoko kwenye kupiga magoti. (Maombi ya Kujidhiri)
- Kupiga magoti huku unasali ni Ishara ya utii na unyenyekevu mbele za Mungu. Mara nyingi wingu la Roho Mtakatifu na nguvu zake huwa linamfunika mwombaji, inayopelekea ububujiko wa nguvu za Ki-Mungu ndani ya mwombaji.
- Kupiga magoti ni Ishara ya uchaji wa Mungu ndani ya mtu anayeomba.
- Unapopiga magoti na kuinama, mara nyingi unampa Roho Mtakatifu kukusemesha jambo. Ufahamu wako na masikio ya kiroho huwa vinakuwa na usikivu wa kiwango cha juu sana. (1Fal 18:42)
- Mungu alimuumba mwanadamu ili apate kushukuriwa na kusifiwa na yeye (Mwanadamu). Unapopiga magoti unapeleka sifa na shukrani mbele zake Mungu.
- Katika kupiga magoti, kunakumwabudu Mungu, kumheshimu Mungu, Kumtukuza Mungu, kuwadhimisha Mungu na Kukubali kwamba Yeye ni Mungu. Ndiyo maana unaweza ukapiga magoti na ukatulia, pasipo kuomba chochote, na ukasikia nguvu fulani inashuka ndani yako. (Luk 22:41, Mdo 7:60, Mdo 9:40, Mdo 20:36)
Angalizo: Usipige magoti endapo mwili umechoka.
    • Mfalme Suleiman: aliomba kwa kuinua mikono yake kuelekea juu mbinuni. (1Fal 8:22)
    • Nabii Ezekiel: alisema mikono yetu tumwinulie Mungu Mbinguni (Maombolezo 4:41)
- Kuinua mikono juu ni Ishara ya utayari wa kufanya kile unachoelekezwa.
- kuinua mikono juu ni ishara ya kujitoa mbele za Mungu.
- kuinua mikono juu ni Ishara ya utayari wa kupokea kile unachokiomba, na kinafanyika sawa sawa na kiu iliyo ndani yako.
- Mikono kuinuliwa wakati wa maombi, ni Ishara ya kuukunjua moyo wako mbele za Mungu na haja zako zote mbele zake.

NB: Usiombe kwa kupiga magoti endapo mwili na akili vimechoka, utalala usingizi wala hutaweza kuomba.

  1. OMBA NA MUZIKI LAINI WA KUMWABUDU MUNGU.
Muziki wa kiroho, na wataratibu, unaweza kukutengenezea mazingira mazuri sana ya kuomba kwa muda mrefu sana. Muziki wa kuabudu, unavuta uwepo wa Mungu kwa namna ya kipekee sana. Neno linasema, ”waimbaji na wanamuziki walipoimba na muziki ukapigwa, nao wakawa kama mtu mmoja, utukufu wa Mungu ukashuka na kulijaza lile hekalu hata makuhani hawakuweza tena kuhudumu” (2Nyak 5:12-14). Kule mbinguni, kila malaika wa sifa ana kinubi (zeze/gitaa). Elisha hakuweza kutoa unabii mpaka mpiga kinubi alipopiga kwa ustadi, ndipo mkono wa Bwana (Roho wa Mungu) alipokuja juu yake, naye akatabiri.
       Nataka uelewe, kwamba kunamuunganiko kati ya muziki wa kiroho na utukufu wa Mungu. Hivyo ukiweza, unapokuwa kwenye mazingira ya kuomba unaweza weka cd au kanda yenye nyimbo za taratibu na za kiroho. Siku hizi asilimmia kubwa simu zetu zinauwezo mkubwa wa kuhifadhi vitu, unaweza ukahifadhi nyimbo nyingi sana, hata kwa kuchukua kwenye mtandao, na zikakusaidia kuvuta uwepo wa Mungu. Utajikuta unaomba kwa muda mrefu sana bila hata kuchoka, na unatamani usiondoke kwenye maombi.

  1. UJUE UNAOMBEA NINI
Biblia inasema ”Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. (Mt 7:7-8). Huwezi kuomba kama hujui unachokiomba (uhitaji wako), huwezi kutafuta kitu usichokijua. Wapo watu wengi sana huwa wanaingia kila siku kwenye maombi, lakini hawana ajenda maalumu wanazoziombea. Biblia inasema ”Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.....Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako” (Isa 41:21; 43:26).
      Mimi huwa ninaziandika ajenda za kuombea, kwenye karatasi dogo tu, na huwa nalishika mkononi, ndipo ninaanza kuombea hizo ajenda, na ninauhakika ninapokuwa naziandika, huwa nakuwa naziandika ndani ya moyo wangu na moyo wa Mungu, maana Yeye najua ndiye aliyeniongoza mpaka nikaziandika. Nikisha anza kuomba naweza nikafunikwa na nguvu kwa namna ya ajabu sana, maana nakuwa niko na mzigo na huku nikinena kwa lugha maana najua Roho Mtakatifu ndiye anayeniombea

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni