KWANINI MUNGU AMEKUPA UZAO?

Mungu aliumba kwanza vitu na wanyama kabla ya mwanadamu, mwanadmu akaumbwa siku ya sita ambayo ilikuwa ni ya mwisho ya uumbaji wake. Mwanadamu aliumbwa siku ya mwisho, bada ya Mungu kuona hana haja ya yeye kukaa hapa duniani na kusimamia kila kitu, akaona ni bora aumbe mtu kwa mfano wake (Mwanzo 1:26), ili vitu vimtambue na vitiishwe chini ya Adamu, Mungu aliamua “kumbarikia”. Neno “kumbarikia” anamaana ni kuviweka vile vitu kuwa chini yake na wengine wabarikiwe kutokana na yeye, pia ni ili Adamu awe na sauti kwa kila kiumbe na kila kitu, na kisiwepo cha kumdhuru.
         Nataka uone jambo fulani kwenye Mwanzo 1:28 inasema:
“Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi”
Angalia mistari mingine kwenye Mwanzo 9:1
Inasema “Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi”
Kusudi lake Mungu ni ili mwanadamu azaliane na kumiliki, kila kitu kiwe chini yake kwa kila kizazi na kizazi. Lakini baada ya dhambi kutokea, tunaona hali ya kutiisha imeondolewa kwa mwanadamu, na kutokea hali ngumu. Na hiyo hali imekuwa ngumu kwa kila mwanadamu, siyo Adamu tu! Na ndiyo maana Kaini na Habili waliamua kuutafuta uso wa Bwana, kwa kutoa sadaka ilimradi waweze kupunguziwa magumu waliyokuwa wanakumbana nayo kutokana na maisha yalivyokuwa chanzo ikiwa ni baba yao (Adamu).
      Adamu ilimgharimu sana baada ya kufa kwa Habili ambaye alipata kibali machoni pa Mungu, ilimgharimu kwa kumtafuta Mungu apate kumleta mwana mwingine, atakaye fanana naye (Adamu) ili Mungu aendeleze kusudi ndani ya mwana aliyesafi.
“Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi” (Mwanzo 5:3)
Mungu alikuwa anahitaji aanze kujitukuza kwa watu kupitia Sethi (Mwanzo 4:26b) “…Hapo ndipo watu walianza kuliitia jina la BWANA” ni baada ya Sethi kuzaliwa. Swali langu, kwa nini Adamu asitubu ili Mungu amtumie yeye watu kuliitia jina la BWANA?
        Nilisikilize itakusaidia sana. Mungu anamweshimu sana mwana, kwani anakuwa anaachilia kusudi fulani ndani ya wana, na ndiyo maana hujaona Adamu baada ya kutenda dhambi akitoa sadaka wala akiutafuta uso wa BWANA, bali Kaini na Habili ndiyo walioingia kwenye kumtafuta Mungu. Nyie wazazi mnapokuwa mnaishi na familia zenu, kumbuka unatakiwa kuishi kwa kumtengenezea mtoto siku zake za mbele (Vision) yaani kila unalolifanya usifanye kwa ajili yako, bali fanya kwa ajili ya watoto wanaokuja kusudi jina la BWANA lizidi kutukuzwa.
".......Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi (wazazi), maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto" (2Kor 12:14b)

        Kama Mungu amekupa uzao na kukupa ahadi za kwenda kuitiisha nchi, inamaana uingie gharama za kumtafuta na kumlea mtoto aliye kama Sethi, kusudi jina la BWANA lianze/liendelee kuitiwa, watu wamjue Mungu kupitia huyo mwana, bali usitengeneze kizazi cha Kaini. Maandiko yanasema “Kaini akaondoka mbele ya uso wa BWANA…”  (Mwanzo 4:16a). Kaini alizaa mpaka vizazi saba na vyote havikumjua Mungu kwa sababu aliondolewa mbele za Bwana, na haikuwa shida ya watoto wake bali ya baba yao (Kaini) kwani hakuingia gharama ya kutengeneza na kutubu baada ya kumuua ndugu yake (Habili) bali alibishana na Mungu kwa lile alilotenda! Angejua Kaini, angewataarifu watoto wake habari za Mungu pamoja na dhambi yake, pengine wangetubu na wangeanza kumtafuta Mungu.
“Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, na watoto wao wakakiambie kizazi kingine”
(Yoeli 1:3)
Panda mbegu ya neno la Mungu ndani ya watoto, ili kizazi na kizazi kipate kuwa na hofu ya Mungu, usitake kuwa kama Kaini, aliyekianzisha kizazi ambacho hakikumjua Mungu.

Si wazazi wengi sana wanaotambua kusudi la Mungu kuwapatia watoto (uzazi), lakini nataka nikupe angalau sababu kidogo:
                                        Itaendelea..................................Barikiwa

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni