Maombi yanaweza kupata “Ndiyo” kama
umeomba sawa sawa na mapenzi ya Mungu, na maombi mengine yanaweza kupata jibu
la “Hapana”, kama hatuyaombi sawasawa na mapenzi yake, au kama Mungu haoni
uzuri wa kutujibu sala zetu kama tulivyoomba, “Na huu ndio ujasiri tulio nao
kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia” (1Yoh 5:14). Biblia inasema: “Hata mwaomba, wala hampati kwa
sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tama zenu” (Yak 4:3). Kila mmoja wetu, anatakiwa kuomba vizuri ili Mungu ampe
jibu la ndiyo na wala si la hapana kwa maombi yake yote. Kuna umuhimu wa
kumtafuta sana
Mungu na kumjua ili upate kufahamu yaliyo mapenzi yake kwako kusudi uombe sawa
sawa na mapenzi yake, “Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu
ni nini yaliyomapenzi ya Bwana” (Efe
5:17).
Mungu anaweza kumpa mtu jibu la hapana
kutokana na hekima yake mwenyewe. Paulo aliomba apone mwiba, au udhaifu wa
afya aliokuwa nao na Mungu akamwambia: “Neema yangu yakutosha; maana uweza
wangu hutimilika katika udhaifu” (2Kor
12:9). Hivyo, Paulo aliendelea kuwa na mwiba huo ila Mungu alimsaidia
kustahimili. Siyo kila uhitaji au masumbufu yanayokukumba ukadhania Mungu
hayaoni, Hapana! Anayaona na anasikia unapokuwa unaomba, lakini anahitaji
uendelee kukaa mbele zake kwani anamakusudi maalumu na wewe, mpaka wakati
utakapofika wa kile alichokukusudia, atakuonesha na kukupatia.
Maombi mengine, yanaweza kupata jibu la
“Subiri”, maana, Mungu kwa hekima yake, anaweza kuona ni vyema mtu asubiri
kwanza, kuliko kumpa jibu la ndiyo wakati huo. Naamini Ibrahimu na Sara
walikuwa wakimwomba Mungu awape mtoto lakini, Mungu aliwapa katika kipindi
alichotaka yeye, Ibrahimu akiwa na umri wa miaka 100 na Sara miaka 90 (Mwa
21:5), japo ahadi ya kumfanya Ibrahimu kuwa taifa kubwa, kwa kupitia uzao wake
ilitolewa wakati Ibrahimu akiwa na umri wa miaka 75 (Mwa 12:1-4). Mfano
mwingine ni huu: kijana mdogo anaweza akamwomba Mungu ampatie mke au mme. Mungu
atamwambia subiri kwanza. Hivyo, tukiona kuwa Mungu hatupi yale tuliyoomba,
tusidhani kuwa Mungu amesema “Hapana” huenda anatutaka tusubiri kwanza.
Mungu pia, anaweza akatupa jibu la “Fanya
hivi kwanza, ndipo upate ulichoomba”. Mfano, yule kipofu aliyeomba aponywe
upofu wake, alipakwa tope machoni, na kuambiwa aende akanawe kwenye bwawa la
Siloamu, ndipo apate kuona (Yoh 9:6-7). Vipofu wengine waliguswa tu na Yesu,
wakaona, na wengine wala hawakuguswa, ila waliambiwa na Yesu, “Imani yako
imekuponya:, nao wakaona, ila huyu alipewa jambo la kufanya kwanza ndipo apate
kuona. Alikwenda kwenye bwawa la Siloamu, lile aliloambiwa na Yesu, aliponawa,
akaanza kuona.
Naamani aliambiwa akaoge mara saba
ndani ya maji ya mto Yordani, ndipo apone ukoma wake (2Fal 5:10). Naamani
hakukubaliana na majibu ya maombi yake, kwa mara ya kwanza, lakini baada ya
kupewa ushauri na kulitimiza lile sharti, la kuoga mara saba akatakasika.
Hivyo, Mungu akituagiza kufanya kitu Fulani kwanza, tukifanye, naye atatufanyia
tuyaombayo.
Mungu pia, anaweza akakujibu maombi
yako kwa kukupa kile unachokiomba, kwa kutegemeana na msimamo wako binafsi,
hata kama siyo mpango wake. Mara nyingi Mungu
hapendi kuingilia maamuzi na misimamo ya mwanadamu, hivyo anaweza akakupa kitu
unachokiomba lakini kikakuharibia maisha yako, “Bali
walitamani jangwani, wakamjaribu Mungu nyikani. Akawapa walichomtaka,
akawakondesha roho zao” (Zab
106:14-15). Mungu huwa anapenda sana
kuonekana kwa mtu amtafutaye kwa bidii, hasa mtu anapoomba jambo Fulani, Mungu
anapenda ajitukuze kwa kumjibu yule mtu, ili kiwango cha imani ya yule mtu
kipande, lakini wengi tunaomba vitu ambavyo siyo wakati wake, wala mazingira
yako kuweza kubeba hicho kitu hauna. Wengi wamefanikiwa, wakaacha hata kwenda
kanisani, wengine wakipata mafanikio wanaanza kunyanyasa wake zao, waume zao,
majirani zao, mpaka ndugu zake. Kwa sababu uko hivyo, basi roho yako itakonda
na hutauona ufalme wa Mungu.
Yapo mambo ya muhimu kuyataja kwenye
sala zetu. Unaposali, usitoe shida zako tu bila ya kusema mambo mengine kwanza.
Anza sala
yako ya kumtukuza Mungu. Sala ya BWANA ni kielelezo chetu. Sala hiyo inaanza kwa
maneno haya: “Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje”
(Mt 6:9). Ni muhimu sana kuanza na kumtukuza Mungu, maana, anastahili
kutukuzwa, na kuhimidiwa, mana bila yeye, hakuna kitu chochote kilichopo
ambacho kingeliweza kuwepo. Yeye ameumba vitu vyote, na anaendeleza kuwepo kwa
vitu vyote.
Baada ya
kumtukuza Mungu, tunatakiwa kuungama dhambi zetu. Kama tutamwomba Mungu, bila ya
kuungama dhambi zetu, Mungu hatasikia, maana dhambi, inaleta utengano kati ya
mtu na Mungu. Yatupasa tuungame, tuwe safi kiroho, ili Mungu wetu, atusikilize
sala zetu. Neno la Mungu linaongea juu ya Mungu kutokujibu sala zetu kwa sababu
ya dhambi zetu kwa kusema: “Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata
usiweze kuokoa; wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu
yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake
msiuone, hata hataki kusikia” (Isa
59:1-2).
Mara
nyingi, sisi wanadamu, huanguka dhambini na dhambi zetu, ndizo zinazotutenga na
Mungu wetu. Yatupasa kukiungama kile kinachotutenga na Mungu kwanza, ili
uhusiano wetu na Mungu urudi, ndipo tumwombe Mungu atusaidie kama yalivyo
mapenzi yake.
Kitu cha tatu kwenye sala, ni kumshukuru Mungu, kwa mema yote
aliyotutendea. Daudi alikuwa akimshukuru Mungu kwenye sala zake. Daudi alitunga
wimbo unaosema: “Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za
milele” (Zab 136:1). Sehemu
nyingine, Daudi alimshukuru Mungu kwa kusema: “Nitakushukuru kwa moyo wangu
wote” (Zab 138:1). Mungu ametutendea
mambo mengi sana. Kama hatutamshukuru katika sala zetu, tutakuwa watu
wasio na shukurani, wasiouhesabu wema wa Mungu kuwa ni kitu chema kwao. Wapo
watu wengi sana, wanaougua, na hata kufa, wengine wanakosa chakula au mahitaji
mengine, na wengi wana shida za kila aina, ila wengine, wanaishi salama. Na
ikumbukwe kuwa, hatuishi salama kwa sababu ya wema wetu, bali fadhili za Mungu,
ni nyingi sana kwetu, hivyo, tunahitajika kumshukuru sana Mungu.
Daudi alipoangalia ulinzi wa Mungu kwake, wema
wake wote aliomtendea, alisema: “Nimrudishie BWANA nini, kwa ukarimu wake
wote alionitendea?” (Zab 116:12). Yatupasa kumshukuru sana Mungu kwa
wema wake wote aliotutendea. Kama hatutamshukuru, tutakuwa kama watu wa siku za
mwisho, “wasio na shukurani” (2Tim 3:2). Watu wanaoona ni haki yao
kufanyiwa, wanayofanyiwa na Mungu, wakati kufanyiwa tunayofanyiwa ni upendeleo,
kwa maana, wazazi wetu walioingia dhambini, waliingia kwa hiari yao wenyewe.
Biblia inasema: “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo
haikutokana na nafsi zetu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye
asije akajisifu” (Efe 2:8). Tunatakiwa kumshukuru sana Mungu kwa yote
anayotufanyia, na wala tusijifanye kama hatuyaoni yale anayotufanyia.
Kitu
cha mwisho cha kutaja kwenye sala zetu, ni
kutoa haja zetu kwa Mungu, ikiwemo na kuwaombea watu mbalimbali pamoja
na wahudumu wa Injili, na wahitajii. Kila mmoja wetu anatakiwa kupeleka
shida zake zote kwa Mungu, maana yeye anaweza kututatulia shida zote, maana
Biblia inasema: “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi
mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye
abishaye atafunguliwa” (Yoh 7:7-8). Lazima tutambue kuwa, hatuwezi kujiokoa
sisi wenyewe, wala kujitatulia matatizo yetu sisi wenyewe (rejea Yoh 15:5).
Yatupasa tumwombe Mungu atusaidie. Ukosefu wa imani kwa Mungu, ndio unaowafanya
watu wengi wasimpelekee shida zao. Tuwe na imani naye, ili tumpelekee shida
zetu, naye atatusaidia, sawa sawa na mapenzi yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni