Daudi alikabiliwa na shida
nyingi sana katika maisha yake. Alipambana na wanyama wakali alipokuwa
akichunga kondoo wa baba yake. Alipambana na jitu Goliathi. Alikuwa auwawe na
Sauli kwa muda wa miaka mingi. Alipinduliwa na mtoto wake Abisalomu, na
kutafutwa auawe na jeshi la Absalomu, na mambo mengine mazito yalimkabili.
Daudi alijifunza njia bora ya kutatua matatizo yake. Shida zake zote,
alimpelekea Mungu kwa njia ya sala.
Akieleza juu ya maombi, Daudi anasema: ”Bwana,
asubuhi utanisikia sauti yangu, asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia”
(Zab 5:3). Daudi alikuwa na kawaida ya kufanya maombi asubuhi, muda ambao bado
bongo zetu zimetulia, wala hazijachoshwa na shughuli za kawaida za maisha. Yesu
alikuwa na kawaida ya kuomba ”alfajiri na mapema sana” (Mk 1:35).
Ni vyema kuwa na muda maalum wa kuomba asubuhi kila siku.
Daudi anaeleza tena namna alivyokuwa
akiomba kwa kusema: ”jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti
yangu” (Zab 55:17). Hapa tunaona jinsi Daudi alivyoomba mara tatu kila
siku ili apate nguvu tele. Ni vema kuongeza muda wa maombi kuliko kuupunguza,
maana mashindano yetu na mwovu Ibilisi, huzidi kuwa makali, amishani mwa mtu, siku
baada ya siku, hasa, anapozidi kumlingana Mungu.
Daudi aliongeza muda wa kumwomba Mungu,
akaomba zaidi ya mara tatu. Biblia inasema: ”katikati ya usiku nitaamka
nikushukuru, kwa sababu ya hukumu zako za haki” (Zab 119:62). Daudi
alikuwa akiomba ”Jioni, asubuhi, na adhuhuri”, baadaye akawa anaomba tena ”Katikati
ya usiku”. Ni vema sana kuwa na maombi mengi zaidi, maana mtu mmoja
alisema: ”maombi mengi, nguvu nyingi za kiroho”. Tuombe sana, tena bila kukoma.
Baadaye Daudi anasema: ”Mara saba kila
siku nitakusifu, kwa sababu ya hukumu za haki yako” (Zab 119:164). Bila shaka
Daudi alimsifu Mungu na kuomba. Hivyo, aliongeza vipindi vya kukutana na Mungu,
akasifu na bila shaka kuomba mara saba. Kadri tunavyoendelea mbele, ndivyo
Shetani anavyoendelea kutusonga na majaribu. Siri ya mafanikio yetu ni kuomba
zaidi na zaidi ili tumshinde Shetani. Anza leo kuwa na muda maalumu wa kuomba
na uombe bila kukoma. Sisi kama binadamu hatuna uwezo wa kumshinda Shetani.
Tunaweza kumshinda kwa uongozi na nguvu za Mungu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni