21.7.14

YATAMBUE MAMBO (7) YA KUCHUNGA SANA UNAPOKUWA KWENYE UCHUMBA/MAHUSIANO

Nilipokuwa nasoma Injili ya Mathayo sura ya kwanza, inaeleza uzao wa Bwana wetu Yesu Kristo tangu Adamu mpaka Yeye. Nikaona kwamba Yesu tunamwita Mwana wa Daudi lakini Daudi hakuwa upande wa Mariamu ambaye alimzaa Yesu, ila Yusufu aliyekuwa mchumba wa Mariamu ndiye aliyekuwa ni wa uzao wa Daudi, na ukiangalia Yusufu naweza kusema hakuusika kwa njia ya damu kwenye uzao wa Yesu bali Mariamu ambaye alikuwa ni mchumba wa Yusufu maana ndyiye aliye tungiwa mimba ya Yesu. Swali langu kulikuwa na nini mpaka Yesu akaitwa mwana wa Daudi? Yusufu na Mariamu walikuwa ni wachumba lakini hawakuwahi kushiriki tendo la ndoa mpaka Yesu anazaliwa, na alizaliwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, sasa ataitwaje Mwana wa Daudi ambaye alikuwa ni upande wa Yusufu?
        Nisikilize! Mbele za Mungu hakuna mchumba bali kuna mke! Kipindi kile Yesu anazaliwa, walikuwepo waliokuwa bikra wengisana na siyo Mariamu peke yake, lakini kwa heshima ya Yusufu na ahadi aliyoitoa Mungu kwamba Bwana Yesu atazaliwa kwenye ukoo wa Daudi, ndiyo maana ikatokea kwa Mariamu ambaye alikuwa ni mchumba (mke) wa Yusufu. Na ndiyo maana nataka uelewe ya kuwa unapokuwa kwenye uchumba, unakuwa tayari upo kwenye mtihani wa kuingia rasmi kwenye uthibitisho wa Mungu, na ndiyo maana unapewa cheti unapofunga tu ndoa kanisani kuthibitisha kwamba umeweza mitihani ya kwenye uchumba. Na mtihani wenyewe ni namna gani unaweza ukaudhibiti mwili wako wakati wa uchumba, ni pale unapotaka kuingilia kusudi la Mungu kwa kutaka kufanya tendo la ndoa kabla ya ndoa.
        
i)                    Mtafute sana Mungu.
Mungu anapokuonesha mke/mume anamaana uendelee kumwobea na kuutafuta uso wa Bwana. Mungu anapoona moyo wako wote na upendo wako wote umehamia kwa huyo mchumba, Mungu anachofanya anawatenganisha kwa kuwafarakanisha, hicho kitu nimekiona kabisa, kuna rafiki yangu alikuwa vizuri sana kiroho alipokuwa akitafuta mke na kweli Mungu akamwonesha na akathibitisha, sasa shida iliyokuwepo ni yule ndugu alipunguza muda wa maombi, akapunguza kusoma neno, hivyo muda wote alikuwa akitumia Simu kuongea na huyo mchumba, mara baada ya miezi miwili akawa ameshuka kiroho kabisa. Mungu alichokifanya akawagombanisha kwa sababu ndogo sana iliyopelekea yule msichana kufikia kusema “sikutaki kabisa” na alidai amepata mtu mwingine, sasa ilimbidi yule kijana aanze tena kuutafuta uso wa Mungu tena, na ilimgharimu sana hadi Mungu kuanza kusema naye kama hapo awali.
         Unapoutafuta uso wa Mungu, Mungu huwa anaachilia hekima namna gani ya kuweza kuishi maisha ya ndoa, unaweza ukawa na umri mkubwa sana lakini huna hekima ya kuweza kulea ndoa na ndiyo maana utashangaa mtu anachumbiwa/anachumbia mara ghafla mambo yanaharibika, ujue Mungu hataki kuaibisha ndoa za Kikristo kwani wengi wakiingia ndani ya ndoa wanashindwa kuwa na hekima namna gani ya kulea hizo ndoa, huwa inakuwa kila siku ni kesi kwa wachungaji mara wazee wa kanisa, kitu ambacho siyo kizuri, hivyo unapopata mwenzi endelea kutafuta mapenzi ya Mungu juu ya hiyo ndoa unayoiendea.
         Tegemea kupata watoto unapoingia kwenye ndoa, kama huna mpango wa kuzaa watoto basi hilo mi sijui, lakini ninalojua moja ya madhumuni ya Mungu kufanya ndoa ni ili watu wakazae na kuongezeka (Mwanzo 1:28) au la uwe na matatizo yako binafsi. Wasichana wengi hasa wa kizazi hiki huwa wanashindwa kuwalea watoto kimaadili, pia hata uvivu wa kuwahudumia vile ipasavyo. Kuna msichana mmoja nikawa namuuliza, hivi wewe katika maisha yako ungependa kuzaa watoto wangapi na kwa muda gani? Akasema kwanza nikiolewa tu nitakaa miaka miwili bila kuwa na mtoto halafu ndipo nitaamua kuzaa, nikamuuliza kwanini? Akasema watoto ni wasumbufu sana! Huyu alionesha uvivu wa hali ya juu sana na hana ujasiri wa kuweza kukabiliana na kila jukumu lililoko mbele yake, ingia kwenye kuutafuta uso wa Bwana ili akupe hekima na ujasiri namna ya kubeba majukumu ya ndoa.

ii)                  Vunja ukaribu.
Usipende kuwa karibu sana na mchuma wako, kwa wale ambao wapo jirani au wanasali kanisa moja, na kwa wale walio mbali, siku hizi kuna Simu hivyo huwa wanaongea sana na kwa muda mrefu kitu ambacho siyo kizuri, mnapokuwa mmekuwa karibu sana kwa namna hiyo huwa Shetani anapata nafasi sana na lazima siku moja mtagombana tu! Tena kwa sababu ya Simu au meseji ama sababu ndogo tu. Kulikuwepo na rafiki yangu ambaye kila siku alikuwa anaongea na mchumba wake hata mara ishirini, kwani ilikuwa kila analofanya huwa anamwambia, sasa kijana wa kiume hakupokea simu mara mbili, yaani kilichofuata ni matusi na kumwambia umenichoka najua unawengine, sasa kwa taaarifa yako hata mimi ninao huku wengi tu! Huyo binti alikuwa akimwambia kijana, basi ikawa ndiyo mwisho wa mahusiano yao.
       Hawa wanaokuwa karibu, mara nyingi sana wanaingia na tamaa ya kufanya uzinzi, nakumbuka kijana fulani mkoa fulani sitaki kutaja, alienda kwa mchungaji na kumwambia uniongoze tena sala ya toba upya kwani nimezini, akasema alikwenda kwa mchumba wake wa kike akaingia mpaka chumbani na akajilaza kitandani, na baadaye alipokuja binti, yule kijana akaingiliwa na tamaa ya kuzini na kwa kumlazimisha yule msichana mpaka wakaweza kuzini, cha kusikitisha, wanasali pamoja na ni wapendwa ambao watu wanawaona wamesimama, na siku hiyohiyo msichana mimba iliingia. Unisikilize msichana, haijalishi unataka uimarishe uchumba au upendo kwa namna gani, maana wengine wanasema nisipomridhisha leo hawazi kunioa, wewe mwambie kama Mariamu kwamba; Yusufu ukiamua kuniacha kwa siri kwa ajili ya Yesu niliyembeba we niache, lasivyo ukubari kunioa na huyu Yesu niliye naye, usikubali kumchafua yesu ndani yako.
       Usikubari mzoeane sana, kwani mtakapoingia kwenye ndoa mtajikuta ni watu kama wa kawaida tu (dada na kaka), kiasi kwamba unatakiwa unapoingia kwenye ndoa kila mmoja anamwona mwenzake kuwa mpya, mkizoeanana sana inafikia baadaye mnakinaiana na mpaka inafikia kudharauliana hatimaye kila mmoja ataanza kuona mwenzake kama siyo chaguo lake mwishowe kuvunjika kwa uchumba.
       Mnaweza mkawa mnafanya kazi ofisi moja, itawabidi mtengeneze nidhamu ya kipekee sana. Nakumbuka tulikuwa nchi fulani sitaki kuitaja, tulikuwa kikazi na tulikuwa watu wengi kidogo kwani tulienda kwa ajili ya semina, sasa katikati yetu kuna watu walikuwa ni wachumba, cha ajabu ni pale wakati wa kwenda kulala, na kwa sababu tulifikia Hotelini ilikuwa ni lazima tulale tofauti tofauti, sasa wao ilikuwa ni kitu kigumu sana ndipo wakataka kutumia nafasi ile kufanya ufuska wao, ikapelekea kila mmoja wetu akagundua ule mchezo waliokuwa wanataka kufanya, mpaka wakakalishwa kikao na wasimamizi. Sasa ni aibu sana kwa picha kama hii na inaonekana nidhamu hawana.

                                                  MWENDELEZO WA SOMO
              Ukisoma Mathayo 1:18-25, Utapata habari za Yusufu na Mariamu mama yake na Yesu, utagundua kwamba baada ya Yusufu kumwona Mariam anaujazito wa Yesu na hawajawahi kukutana kimwili, lile jambo lilimfanya Yusufu aanze kumwacha kwa siri Mariamu. lakini kile kitendo cha Yusufu kutaka kumwacha Mariam kilimpa Mungu nafasi ya kumthibitishia Yusufu uchumba wao, na Mungu alisema usimwache mkeo! na Yusufu akajirudi, lakini fikiria Yusufu angeamua kukaa tu naye kwa sababu ya kupenda lakini akiwa na kinyongo ndani yake kwamba Mariam amepata mimba nje ya ndoa ingekuwaje! Mungu aliamua kusema kwa sababu Yusufu alijaribu kujitenga na Mariamu. hivyo unapovunja ukaribu na mchumba wako inampa nafasi Mungu kusema na kufanya jambo katika mahusiano yenu, na kama siyo wa kwako itajulikana hapo. wengi wameoana na siyo makusudi ya Mungu bali ni kwasababu walijiambatanisha wao kwanza na Mungu akawa hana nafasi ya kusema nao.


iii)                    Ukweli na uwazi
Wakati wa uchumba ndiyo kipindi ambacho utatakiwa kumchunguza na kumfahamu mwenzi wako, wapi ni mdhaifu na wapi yupo imara, kusudi ujipange namna gani ya kumsaidia pindi utakapoingia kwenye ndoa, na endapo mwenzako hatakubaliana na udhaifu utakaokuwa nao, basi huyo Mungu hakukusudia mje kuishi pamoja. Kijana mmoja tulikuwa wote chuoni, alikuwa na mchumba wake na wote wameokoka vizuri sana, sasa ghafla akaja akaniambia “nataka nikwambie kwamba fulani siyo mchumba wangu tena!” Mi nikashangaa, kwani hawa watu tayari hata nyumbani kwao wanatambuana, aliponipa sababu akasema mimi sikujua kwamba mtu mzima kama yule anaweza akawa anakojoa kitandani, na juzi ndiyo nimejua napo hajaniambia yeye! Nikashangaa sana kiasi kwamba nikaona kwamba Mungu hakupanga hawa wawili waje kuishi pamoja, kwani hiyo ni sababu ndogo sana, na inamana angekuwa ni yeye je!
       Kuna mambo mengine ambayo ni muhimu wakati wa uchumba kuweza kuambiana ukweli na mengine siyo uyafunue, haswa ya kifamilia. Ndoa nyingi zimekuja kusumbua kwa sababu baada ya kuingia kwenye ndoa ndipo unakuja kutambua kwamba kumbe mmojawapo anamtoto tayari huko nje, na hakukwambia mpaka mmekuja kufunga ndoa. Huwa yanatokea sana siku hizi, na kwa sababu vijana wengi wanaonana mjini au chuoni, ghafla wanapendana na wanafikia mpaka ndoa hata bila kujua historia ya mwenzake huko walikotoka. Fikiria ndiyo mnaenda kusalimia na kutambulishana kwa wazazi kijijini baada ya kuoana, sasa ndiyo unakutana na familia ya huyo mwanamke/mwanaume si utazimia!

iv)                  Usitumie udhaifu wa mwenzio
Uchumba siyo kuumizana, msiingie kwenye ndoa mkiwa na vidonda vilivyotokana na kipindi cha uchumba. Hizi hali huwa zinatokea sana, kijana wa kiume anapoufunua upendo wake kwa msichana, na pindi msichana anapotambua kwamba anapendwa sana na mchumba wake, huwa kinachotokea yule msichana anadiriki kumwendesha mwenzake kwa kila hali, analosema anataka ndivyo iwe hivyo. Muda mwingine anajaribu mpaka kumwmbia ya kwamba mi ntakuacha endapo wakizozana kidogo, sasa vitu kama hivyo baadaye vinaleta athari kwenye ndoa. Kuna ndoa niliwahi kuiona mkoa fulani yaani mwanamume anapigwa na mke wake, kisa yule mwanamke alikuwa ni mzuri sana wa sura, sasa mume wake alikuwa amempenda sana mke wake hivyo anaona bora apigwe tu lakini mke aimwache. Ndoa nyingine niliona mwanamke alikuwa na hela kuliko mwanamume, sasa inapofikia wakati wa kupika chakula alikuwa anaambiwa mwanamume akapike.
      Mshukuru Mungu pale mwenzio anaonesha upendo wa dhati kwako, nawe jitahidi uoneshe upendo kwake, kunawengine wanatamani sana kusikia hata neno “I love you”  kwao ni adimu sana. Sasa wewe unaambiwa kila dakika hayo maneno na yanakupa kiburi cha kumnyanyasa mwenzako, muda mwingine unaweza ukawa unajaribu kama kumpima, lakini kumbe nawe unampenda kweli, sasa siku akaamua kukata tama na mawasiliano ndipo utakapotambua thamani yake.
“Mwanamke akamwambia, wawezaje kusema nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi” (Waamuzi 16:15)
Ni habari za Samsoni na Delila, na maneno hayo alikuwa akiyasema Delila akimwambia Samsoni pale alipokuwa anahitaji kujua asili ya nguvu zake, hivyo Delila alijua hana namna yoyote ile ya kumbana Samsoni ili aseme asili ya nguvu zake, lasivyo amwambie suala la upendo kwamba akiendelea kumdanganya basi Delila ataachana na Samsoni, na kwa sababu Samsoni alimpenda sana Delila hivyo ilimlazimu Samsoni kumwambia siri ya nguvu zake. Ndivyo ilivyo siku hizi, kijana akimpenda sana msichana huwa anabanwa sana mpaka hela zote zinakwenda kwa msichana hata kabla ya ndoa.

         Wasichana wengine huwa wanapokuwa na marafiki zao, huwa wanatabia ya kulingishiana wachumba zao, kwamba yupi anapendwa sana na mchumba wake. Wanafikia mpaka kushindana kwamba “mimi wa kwangu ana hela, nikimwomba hata saizi alfu hamsini anatuma” na wanaamua kuomba kwa huyo mchumba wake, na asipotumiwa atakuwa ameaibisha na anajikuta anaingi kumchukia mchumba wake kwa sababu ya kijinga. Na uelewe unapojitangazia kwa wenzako kwamba unapendwa sana, sasa kwa taarifa yako kunawasichana wanamapepo ya kupenda wanaume wa wenzao, utashangaa kesho mchumba wako yupo na rafiki yako.

INAENDELEA





 +255 (0) 712 201 073/ +255 (0) 752 005 418

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni