Nini Maana ya Wokovu?

Siyo busara kusema kwamba "hakuna kuokoka, haiwezekani kuokoka," huku hatujui hata maana ya kuokoka. Mtu mwenye busara kwa mfano, hawezi kusema hakuna ”Nguvu ya Uvutano“ huku hajui hata maana ya nguvu hiyo. 
  
Watu wengi watajikuta wanakwenda katika mateso ya Jehanam ya moto, kwa sababu tu hawajui maana ya kuokoka, na jinsi ya kuokoka katika mateso hayo. Sasa basi, ni nini maana ya kuokoka?

Kuokoka au kuokolewa, ni kunusurishwa, kuopolewa, kusalimishwa au kuponywa kutoka katika maafa makubwa yaliyo dhahiri kabisa kumpata mtu.

Inaweza ikawa kuponywa kutoka katika hatari ya kifo, adhabu kali au madhara yoyote makubwa yaliyo dhahiri. 
Katika hali ya kukosa matumaini ya kukwepa maafa hayo yaliyo dhahiri, inapotokea ghafla njia ya kusalimika; hapo tunasema mtu aliyesalimika au kunusurika, ameokoka. Kwa mfano, mtu asiyejua kuogelea anapotumbukia baharini baada ya mashua aliyokuwa anasafiria kupinduka, halafu akaanza kunywa maji, na kuwa katika hatari ya kufa maji; anapotokea bingwa wa kuogelea, na kumsalimisha mtu wa jinsi hiyo, hapo tunasema kwamba bingwa wa kuogelea, amemuokoa mtu huyo, na mtu huyo ameokolewa au ameokoka.

Miaka kadhaa iliyopita  katika nchi yetu ilitokea ajali mbaya ya meli ”Mv Bukoba.“ Meli hiyo ilizama  katika Ziwa Victoria ikiwa na abiria; na mamia kwa mamia walikufa maji .Meli hiyo ilipinduka na kuzama, ikiwa chini juu. Mpaka leo, haikuwezekana kuitoa ile meli majini, na hivyo mamia hao ”walizikwa“ katika meli hiyo. Yalikuwa ni maombolezo makubwa ya kitaifa. Ninamfahamu dada mmoja ambaye alikuja kuniona, ili nimwombee kwa Mungu; apate faraja, na kutoka katika hali ya mawazo mengi. Dada huyu alifiwa na ndugu zake 22, kwa mpigo, na wote walizama  katika meli hiyo, na hakuna hata mmoja aliyepatikana hata mwili tu wa kuzika. Ndugu hawa wote walijikusanya Dar-Es-Salaam, Dodoma, Tabora na Mwanza na kwenda Bukoba kwenye msiba.

Baada ya msiba, wakaamua wote kwa pamoja kurudi kwa meli hiyo, siku hiyohiyo moja. Matokeo yake, ikawa ni  kupata ajali hiyo na kufa maji. Hata hivyo, pamoja na mamia kwa mamia kufa maji katika ajali hiyo mbaya, wako watu wachache ambao walinusurika kufa. Vyombo vya habari vilipokuwa vikitoa taarifa hii, vilisema ”Watu waliookoka katika ajali ya ”Mv Bukoba“, waelezea mkasa uliowapata“. Wale walionusurika katika ajali hiyo, walisemekana wameokoka.

Baada ya kuelewa maana ya neno ”Kuokoka“, hatuna budi kufahamu kwamba, neno ”kuokoka“, linatumika kwa maana hiyohiyo, linapokuwa linahusishwa na ”walokole.“ Labda utaniuliza, ”Kwa vipi walokole wameokoka? Wamenusurika katika mkasa upi?“ Katika kujibu swali hili, unahitajika ufafanuzi wa kina ili tupate kuelewa. Tufuatane sasa hatua kwa hatua, ili upate kuelewa.   

Wanadamu wote ni wenye dhambi kutokana na asili yetu. Kutokana na mzazi wetu Adam aliyefanya dhambi, sisi sote tunazaliwa tukiwa na asili ya dhambi na hivyo kujikuta tunatenda dhambi. Kwa mtu mmoja (Adam), dhambi iliingia ulimwenguni na kila mmoja wetu anahesabiwa kuwa na dhambi (Warumi 5:12). Biblia inasema katika Zaburi 51:5, ”Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani.“ Sisi sote, tunazaliwa tukiwa na asili ya dhambi. Ndiyo maana utaona mtoto mdogo anasema uongo, ana hasira, wivu n.k. Mtoto mdogo akisikia muziki wa dansi, atakata viuno na kucheza, bila hata kufundishwa. Mtoto mdogo akinyimwa au kucheleweshwa ”nyonyo“ au kunyonya ziwa la mamaye, atakasirika na kumpiga mamaye kofi pamoja na kamkono kake kadogo. Hasira hii imetoka wapi? Ni kutokana na dhambi ya asili ya Adam.

Hivyo kutokana na asili ya dhambi, kila mtu anahesabiwa kuwa ni mwenye dhambi; awe anavuta sigara au havuti sigara. Awe anakunywa pombe au hanywi pombe. Awe anafanya uasherati  au hafanyi uasherati. Awe anafanya dhambi hii au nyingineyo, bado kila mwanadamu ni mwenye dhambi. Awe anafanya dhambi nyingi au chache, hiyo haijalishi, bado mwanadamu ni mwenye dhambi kutokana na asili yake. Mnazi unabaki mnazi, ukitoa nazi elfu moja, nazi kumi au usipotoa nazi kabisa. Mnazi, ni mnazi, kutokana na asili yake ya mti.  Mwanadamu yeyote, hata akijitahidi kutenda mema, ni kazi bure, bado mbele za Mungu, anahesabiwa kuwa hana haki, ni mkosaji, kutokana na asili yake ya dhambi.Tunasoma katika AYUBU 9:29-31, Nitahukumiwa kuwa ni mkosa; Ya nini nitaabike bure?  Ingawaje najiosha kwa maji ya theluji,na kuitakasa mikono yangu kwa sabuni; lakini utanitupa shimoni.“  Tena tunasoma katika ISAYA 64:6, ”Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi.“

Sasa basi, matokeo ya dhambi ni nini? Ni adhabu. Hakuna mwenye dhambi atakayekosa adhabu. Lazima kila mwenye dhambi atapata adhabu ya milele yaani kutupwa katika ziwa la moto na kutengwa na Mungu milele (WARUMI 6:23; UFUNUO21:8). Hakuna mtu yeyote mwenye dhambi, yaani asiyekuwa na haki mbele za Mungu atakayeokoka katika adhabu hiyo. Biblia inasema katika ZABURI 119:155, ”Wokovu u mbali na wasio haki“.Kutoa sadaka nyingi, kusali mara tatu au mara tano kwa siku, kuimba kwaya, kipaimara, ubatizo wa utotoni au tendo lolote linaloonekana jema kidini, haliwezi kumfanya mtu anusurike katika adhabu hii ya moto wa milele. Hata kama mtu hanywi pombe, havuti sigara au siyo mwizi, bado tu atakwenda katika moto wa milele kutokana na asili ya dhambi iliypmo ndani yake. Dhambi ya asili ya Adamu, inatosha kabisa kumtupa mtu katika moto wa milele bila nyongeza yoyote ya dhambi.

Wokovu u mbali kabisa na wasio haki, na hakuna mwanadamu mwenye haki mbele za Mungu (AYUBU 25:4). Ili mtu aokoke kutoka katika adhabu ya moto wa milele, lazima kwanza ahesabiwe na Mungu kuwa ni mwenye haki. Biblia inasema katika MITHALI 11:21, ” Hakika mtu mwovu hatakosa adhabu; bali wazao wa wenye hakiwataokoka“. 

Unaona sasa? Ili mtu anusurike au aokolewe kutoka katika adhabu ya moto wa milele, ni lazima kwanza ahesabiwe haki  ya kuingia mbinguni, na Mungu mwenyewe. Mwanadamu anahesabiwa haki namna gani na kuokoka? Hatuhesabiwi haki na Mungu kwa kujitahidi kushika nguzo fulani za dini, kwenda Jumapili Kanisani, kujaribu kuishika sabato, kufanya sakramenti zote au matendo ya sheria. Tunahesabiwa haki kwa imani tu! Kwa imani tu, mtu husafishwa dhambi zake kwa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani, na Mungu mwenyewe humpa uwezo wa kushinda dhambi, na kumuwezesha kuishi maisha ya utakatifu. Biblia inasema katika WARUMI 3:28, ”Basi twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria“.

Je, mtu anaweza kuokoka akiwa hapa duniani?
Tukijaribu kujitahidi kuacha pombe, sigara au dhambi yoyote, kwa nguvu zetu, hatuwezi! Kwa kujitahidi kwa nguvu za kibinadamu, hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuishi maisha ya utakatifu hapa duniani. Ndiyo maana watu wamekata tamaa  na kusema kwamba haiwezekani mtu kuokoka duniani, eti wokovu ni mpaka mbinguni. Je, kuna ukweli katika maneno hayo ? Jibu ni la! Kuokoka ni hapa hapa duniani, siyo mbinguni! Ziko sababu kadha zinazothibitisha kwamba kuokoka ni hapa duniani. 

Kwanza, Yesu Kristo alitoka mbinguni na kuja duniani kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. Biblia inasema katika LUKA 19:10, ”Kwa kuwa Mwana wa Adam alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.“ Kama wokovu ungekuwa hukohuko mbinguni baada kufa, Yesu asingekuwa na haja ya kuja huku duniani. 

Pili, Yesu alipokuwa katika safari zake za injili, akiwa duniani, wakati mmoja aliingia katika nyumba ya mtu mmoja aliyeitwa Zakayo na kumwambia,  Leo wokovu umefika nyumbani humu.“ (LUKA 19:9). Kama mtu angekuwa anaokoka baada ya kufa, Yesu asingetumia neno, ”Leo“. 

Tatu, Neno la Mungu linasema Mungu anapendezwa na watakatifu walioko duniani. Tunasoma katika ZABURI 16:3, Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, hao ndio ninaopendezwa nao“.  Neno pia, linasema wazi kwamba tunapaswa kuishi kwa kiasi na utauwa, yaani utakatifu, katika ulimwengu wa sasa  (TITO 2:11-12). 

Nne, kwa sababu wokovu ni hapa duniani, ndiyo maana Yesu alipokuwa duniani aliwahubiri watu waokoke hapahapa  duniani. Kwa maneno yake akihubiri katika YOHANA 5:34, anasema ”Walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka.“

Tano, watu waliokuwa duniani walishuhudia kwamba waliokolewa na kuacha dhambi hapahapa duniani. Hawa wanasema katika TITO 3:3-4, Maana hapo zamani, sisi nasi tulikuwa hatuna akili tulikuwa waasi, tumedanganywa huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi (duniani), tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana. Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu ulipofunuliwa (kwetu), alituokoa.“ Unaona hapa! Wanatumia maneno, ” Hapo zamani“, na ”Tulikuwa“, wakizungumzia maisha yao ya uovu ya muda uliopita na tena wanatumia neno, ”Alituokoa“, linalozungumzia jinsi walivyookolewa muda fulani uliopita; ingawa bado walikuwa hapahapa duniani.

Kwa nini watu wanasema haiwezekani kuokoka hapa duniani? Kama tulivyogusia kitambo, ni kwa sababu watu wanafikiri kwamba wanaweza kuishi maisha ya utakatifu kwa kujitahidi kwa nguvu zao. Watu waliokata tamaa na kuona kwamba haiwezekani kuishi maisha ya utakatifu hapa duniani, wamejaribu kutumia nguvu za kibinadamu! Jambo hili linaelezwa vizuri katika MATHAYO 19:25-26, ” Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema Ni nani basi awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani, bali kwa Mungu yote yanawezekana.“ Kwa uwezo wa kibinadamu, hatuwezi kuokoka hapa duniani, lakini kwa uwezo wa Mungu jambo hili ni rahisi sana. Uwezo wa Mungu ulimbadilisha Sauli aliyekuwa mwuaji, na kumfanya Mtume. Sisi nasi kwa imani tu tunapotubu dhambi na kuziacha, tunapata rehema ya kusamehewa dhambi zetu na kupata uwezo wa kushinda dhambi duniani aliokuwa nao Yesu Kristo (MITHALI 28:13; WAEBRANIA 4:14-16).

Ni muhimu kufahamu kwamba mtu yeyote akimwendea Yesu, kwa imani, na kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha, atasamehewa dhambi zake mara moja maana neno lake linasema katika YOHANA 6:37, ”… wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.“ Hata kama dhambi zetu ni nyingi kiasi gani, Yeye hutusamehe mara moja (ISAYA 1:18). Siyo hilo tu, nimuhimu kufahamu kwamba msamaha huu wa dhambi huambatana na wokovu! Biblia inasema katika LUKA 1:17, ”Uwajulishe watu wake wokovu, katikakusamehewa dhambi zao.“ Ukisamehewa dhambi zako, kwa ghafla tu, utaona kiu yote ya dhambi imehama kabisa na unapenda tu kufanya mapenzi ya Mungu, huku ukiwa na uwezo wa kushinda dhambi. Je, unapenda kuokoka leo? Najua unapenda. Basi, kwa imani fuatisha sala hii, 
  
"Mungu Baba, ninashukuru kwa ujumbe huu. Ninatubu dhambi zangu kwa kumaanisha kuziacha. Yesu Kristo naomba unisamehe dhambi zangu zote za kuzaliwa na kutenda. Nisafishe dhambi  zote kwa damu yako iliyomwagika msalabani na kunipa uwezo wa kushinda dhambi na kuniokoa. Asante kwa kuniokoa, katika Jina la Yesu. Amen.“  
  
Tayari sasa umeokoka. Ili uzidi kuukulia wokovu ulioupokea leo, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI!!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni