- TAFUTA MAHALI PAZURI PENYE UTULIVU. (Marko 1:35)
Ili uweze kuomba kwa utulivu na kwa umakini, chagua au
tafuta mahali pazuri patakapokupa utulivu katika kuomba (Concentration in
prayer). Ndio maana Mungu alipenda kuongea na Musa mlimani, (Kutoka 24:12-18).
Hata Yesu alizoea kwenda kuombea mlimani, mahali palipo mbali na vurugu za
watu, alipenda kwenda mlimani, (Mathayo 14:22-23). Tafuta mahali patulivu;
chumbani, kanisani, mlimani, n.k (Mt 6:5-6).
- TENGA MUDA MZURI (Mhubiri 3:1-7)
Ukitaka uombe kwa umakini mzuri, chagua muda mzuri ambao
utakuwa unahakikisha akili yako na mwili wako viko freshi. Usije ukalazimisha
kuomba hata kama akili yako au mwili wako umechoka sana. Kila jambo lina wakati
wake. Kama umechoka sana, huo si muda wa kuomba, bali ni wa kupumzika.
Usilazimishe ratiba. Ni bora upumzike ili baadaye uweze kuomba vizuri. Usije
ukajikuta unapiga tu miayo na hujui unaomba nini. Penda kuomba wakati unanguvu
ya akili na mwili, ili uwe makini kuongea na Mungu kwa akili timamu. Ndio maana
Yesu alipenda kuamka alfajiri sana kwenda kuomba mlimani. Hakikisha kazi za
muhimu umezimaliza, usije ukawa unawaza mboga jikoni, mara mtoto hajaoga, sijui
tutakula mboga gani, hapana! Weka mipango ya kazi zako vizuri, ili ukianza kuomba
hivyo vitu visiingilie kati.
Hata
nyumbani, jaribu kutenga muda wa kuangalia TV, na siyo muda wote unatazama TV
mpaka inakuondolea mawazo ya kuomba. wengine huwa wana muda maalumu wa
kutazama, ni tarifa ya habari saa 2 usiku mpaka saa 3:30 ndipo wanazima, na
kuendelea na ratiba zingine. Nidhamu ya kumtafuta Mungu kwa kumtengea muda wa
kuongea naye ni vizuri zaidi kwani itakutengenezea heshima mbele zake. Biblia
inasema ”nawapanda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii watanina”
Mith 8:17. ukimheshimu Mungu kwa kutenga muda kwa ajili yake, na yeye
atakuheshimu.
- OMBA KATIKA ROHO (Nena kwa Lugha). (Rum:26-27, Waefeso 6:18)
Kuomba kwa Roho, yaani kunena kwa Lugha, kunamfanya Roho
Mtakatifu anayejua kuchunguza mioyo yetu na haja tulizonazo, anakamata ulimi
kuhakikisha anakuombea vile Mungu atakavyo, na kwa kutegemeana na mzigo ulionao
mpaka uishe ndani yako ndipo anakuachia. Hivyo kwasababu mahitaji tunayomengi,
huwa unaweza ukajikuta unaomba kwa muda mrefu zaidi mpaka Mungu aone mpenyo wa
kuachilia ukiombacho. Tunapoomba kwa akili za kibinadamu, mungu anasikia pia,
lakini maombi yako yanakuwa na mipaka, kwa sababu akili ya mtu haijui kila
kitu. Bali Roho wa Mungu anajua kila kitu. Naye hutupa kipawa cha kuomba kwa
lugha ya mbinguni iliyo bora zaidi. (Yuda 1:20, Marko 16:17, 1Kor 14:1-4,
15-16,7)
Unaponena
kwa lugha, unaalika nguvu nyingi za Mungu na malaika wanakuzunguka, kwani lugha
inayotumika ni lugha ya malaika (1Kor 13:1), hivyo hufuata pale palipo na uwepo
wa mtu anayewasiliana nao, ingawa mwombaji hawezi kuwaona. Wanasaidia kumpinga
shetani asizuie maombi ya mwombaji na asiweze kuelewa neno lolote liombwalo.
- WAKATI MWINGINE OMBA KWA KUFUNGA (Mathayo
6:16-18)
Kufunga kunasaidia kudhoofisha mwili, ili roho iwe makini
zaidi kuongea na Mungu kwa kina zaidi. Mwili huu siku zote haupendi kufanya
mambo ya Mungu. Unapofunga, unajionesha mbele za Mungu kujitoa kwako kama
dhabihu iliyo hai. Unampa Mungu kipau mbele kuliko vyote, ni badala ya kutoa
sadaka ya pesa au ya aina yoyote, kwani kule kuomba tu ni sadaka tosha mbele za
Mungu (Mith 15:8). Kama Yesu alivyojitoa kuwa dhabihu takatifu kwa Mungu kwa
ajili ya mwanadamu, ndivyo vivyo hivyo, unapofunga unajitolea kwa ajili yako na
kwa niaba ya wengine, (Isaya 58).
Mara
nyingine, kama unapenda kufanya ibada jioni, pengine majira ya saa 2 usiku, kwa
watu wengi muda huo unakuwa ni muda wa chakula cha jioni. Lakini nataka
nikwambie kamba, mtu akisha shiba huwa mwili unachoka na kupelekea kulala
(unalewa). Kwenye chakula kunamchanganyiko wa vitu vingi ambavyo vipo kwenye
chumvi ama sukari. Mfano ukinywa chai ni lazima usikie kulala tu! Kwani kuna sulpher ambayo inapelekea kulewa kwa akili na mwili. Ndiyo
maana ukishiba tu, unasikia kulala.
Ukiweza,
jifunze kula vizuri mchana, ama majira ya saa kumi jioni, halafu majira ya saa
moja au saa mbili, uweze kutumia matunda mchanganyiko, wala chai usitumie. Hiyo
itakusaidia kuweka mwili kuwa mwepesi sana na kusikia kuchangamka, ambapo
utaweza kukaa muda mrefu pasipo kulala.
- MARA NYINGINE OMBA NA RAFKI YAKO. (Mhubiri
4:9-10)
Biblia inasema ”Ni heri wawili kuliko mmoja”. Kuna faida ya kuomba pamoja na rafiki yako. Kwanza,
mnapokuwa wawili au watatu, inaleta hamasa na hari ya kuomba zaidi. Si rahisi
kujisikia mvivu unapokuwa na waombaji wenzako. Pili; nguvu ya kiroho
inaongezeka. Neno linasema, mwombaji mmoja anafukuza adui elfu moja,
bali wakiwa wawili, wanafukuza elfu kumi, (siyo elfu mbili! Ni elfu
kumi!, (Kumb 32:30). Hiyo ni kanuni ya mbinguni/Ki-Mungu. Kadri mnavyoongezeka,
ndivyo na nguvu ya Mungu inaongezeka.
Hivyo,
wakati mwingine omba na rafiki yako unayemwamini, unayeweza kumshirikisha mambo
yako ya binafsi. Mashujaa wengi wa imani, walikuwa na marafiki zao wa kiroho.
Mfano:- Mathayo 17:1-9.
§
Musa
– alikuwa na Joshua, Haruni na Huri.
§
Eliya
– alikuwa na Elisha
§
Elisha
– akaja akawa na Gehazi
§
Danieli
– alikuwa na Shadrack, Meshack na Abednego.
§
Yesu
– alikuwa na Petro, Yakobo na Yohana.
§
Paulo
– alikuwa na Barnaba, Timotheo na Tito.
Kama huna rafiki wa karibu wa kuomba naye, usikurupuke kujichagulia. Tulia
umwombe Mungu akupe mtu atakayekuwa msaada kwako. Mtu mtakayefungamanishwa naye
katika roho, hata kama mko mbali mbali kijiografia, lakini katika roho mko na
umoja mzuri wa imani. (Mathayo 18:18-19)
- ITAMBUE MIKAO
INAYOKUPA UHURU NA UPAKO UNAPOOMBA.
Kila mtu ana namna yake alivyozoea akiwa anaomba, lakini
kunamikao mingine ambayo ukijifunza/ukaiiga, inakupa upako, kutegemeana na
uelewa wa huo mkao unamaanisha nini mbele za Mungu. Katika kuomba kwa muda
mrefu, mkao uliouzoea utakusaidia kwenda mwendo mrefu au mfupi. Yakupasa kujua
nguvu yako na udhaifu wako. Wakati wa kuomba, epuka mikao inayokuchosha haraka
na tumia mikao inayokupa nguvu zaidi. Kwa mfano, ukiwa umechoka usipende kuomba
kwa kupiga magoti au kuegemea kitandani, au kukaa chini ama popote. Ni bora
uombe ukiwa umesimama au unatembea tembea, ili kuepusha usingizi na uchovu. Waliozoea
maombi wengine huwa wanabadilisha badilisha mikao ili isiwachoshe.
Mifano ya waombaji walioomba kwa mikao tofauti na kwa sababu za Ki-Mungu.
- Mzee Ibrahimu: aliomba kwa kusimama, (Mwanzo 18:22)
- Kusimama, maana yake kuutambua wajibu wako, kwenye eneo
lako, muda wako maalumu, na kile unachotakiwa kusimamia, vikiwemo ahadi na
mpango wa Mungu juu ya ukiombacho. (Habakuk 2:1)
- Daniel:
aliomba kwa kupiga magoti. (Dan 6:10)
- Mtume
Paulo: aliomba kwa kupiga magoti (Efeso 3:14)
- Bwana
Yesu: aliomba kwa kupiga magoti. (Luka 22:41)
Nguvu iliyoko kwenye kupiga magoti. (Maombi ya
Kujidhiri)
- Kupiga magoti kwenye maombi, ni Ishara ya utii na
unyenyekevu mbele za Mungu. Mara nyingi wingu la Roho Mtakatifu na nguvu zake
huwa linamfunika mwombaji, inayopelekea ububujiko wa nguvu za Ki-Mungu ndani ya
mwombaji.
- Kupiga magoti ni Ishara ya uchaji wa Mungu ndani ya mtu
anayeomba.
- Unapopiga magoti na kuinama, mara nyingi unampa Roho
Mtakatifu kukusemesha jambo. Ufahamu wako na masikio ya kiroho huwa vinakuwa na
usikivu wa kiwango cha juu sana. (1Fal 18:42)
- Mungu alimuumba mwanadamu ili apate kushukuriwa na
kusifiwa na yeye (Mwanadamu). Unapopiga magoti unapeleka sifa na shukrani mbele
zake Mungu.
- Katika kupiga magoti, kunakumwabudu Mungu, kumheshimu
Mungu, Kumtukuza Mungu, kumwadhimisha Mungu na Kukubali kwamba Yeye ni Mungu.
Ndiyo maana unaweza ukapiga magoti na ukatulia, pasipo kuomba chochote, na
ukasikia nguvu fulani inashuka ndani yako. (Luk 22:41, Mdo 7:60, Mdo 9:40, Mdo
20:36)
- Mfalme Suleiman:
aliomba kwa kuinua mikono yake kuelekea juu mbinuni. (1Fal 8:22)
- Nabii
Ezekiel: alisema; mikono yetu tumwinulie Mungu Mbinguni
(Maombolezo 4:41)
- Kuinua mikono juu ni Ishara ya utayari wa kufanya kile
unachoelekezwa kufanya.
- kuinua mikono juu ni ishara ya kujitoa mbele za Mungu.
- kuinua mikono juu ni Ishara ya utayari wa kupokea kile
unachokiomba, na kinafanyika sawa sawa na kiu iliyoko ndani yako.
- Mikono kuinuliwa wakati wa maombi, ni Ishara ya
kuukunjua moyo wako mbele za Mungu na haja zako zote mbele zake.
NB: Usiombe kwa kupiga magoti endapo mwili na akili
vimechoka, utalala usingizi wala hutaweza kuomba.
- OMBA NA MUZIKI LAINI WA KUMWABUDU MUNGU.
Muziki wa kiroho, na wataratibu, unaweza kukutengenezea
mazingira mazuri sana ya kuomba kwa muda mrefu sana. Muziki wa kuabudu, unavuta
uwepo wa Mungu kwa namna ya kipekee sana. Neno linasema, ”waimbaji na wanamuziki
walipoimba na muziki ukapigwa, nao wakawa kama mtu mmoja, utukufu wa Mungu
ukashuka na kulijaza lile hekalu hata makuhani hawakuweza tena kuhudumu”
(2Nyak 5:12-14). Kule mbinguni, kila malaika wa
sifa ana kinubi (zeze/gitaa). Elisha hakuweza kutoa unabii mpaka mpiga kinubi
alipopiga kwa ustadi, ndipo mkono wa Bwana (Roho wa Mungu) alipokuja juu yake,
naye akatabiri.
Nataka
uelewe, kwamba kunamuunganiko kati ya muziki wa kiroho na utukufu wa Mungu.
Hivyo ukiweza, unapokuwa kwenye mazingira ya kuomba unaweza weka CD au kanda
yenye nyimbo za taratibu na za kiroho. Siku hizi asilimmia kubwa simu zetu
zinauwezo mkubwa wa kuhifadhi vitu vingi, unaweza ukahifadhi nyimbo nyingi
sana, hata kwa kuchukua kwenye mtandao, na zikakusaidia kuvuta uwepo wa Mungu.
Utajikuta unaomba kwa muda mrefu sana bila kuchoka, na unatamani usiondoke
kwenye maombi.
- UJUE UNAOMBEA NINI
Biblia inasema ”Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi
mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye
atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. (Mt 7:7-8). Huwezi kuomba
kama hujui unachokiomba (uhitaji wako), huwezi kutafuta kitu usichokijua. Wapo
watu wengi sana huwa wanaingia kila siku kwenye maombi (au kwa kuamka usiku),
lakini hawana ajenda maalumu wanazoziombea, ndiyo maana wanakuwa hawana msukumo
wa kuomba. Biblia inasema ”Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA;
toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.....Unikumbushe, na
tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako” (Isa 41:21;
43:26).
Mimi huwa
ninaziandika ajenda za kuombea, kwenye karatasi dogo tu, na huwa nalishika
mkononi, ndipo ninaanza kuombea hizo ajenda, na ninauhakika ninapokuwa
naziandika, huwa nakuwa naziandika ndani ya moyo wangu na moyo wa Mungu, maana
Yeye najua ndiye aliyeniongoza mpaka nikaziandika. Nikisha anza kuomba naweza nikafunikwa
na nguvu kwa namna ya ajabu sana, maana nakuwa niko na mzigo na huku nikinena
kwa lugha maana najua Roho Mtakatifu ndiye anayeniombea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni