Usomi wa ngazi mbalimbali si sifa ya mtu kufaa kuwa kiongozi, dunia
katika historia yake ina majina lukuki ya baadhi ya viongozi ambao
walikuwa wasomi, lakini hatima ya uongozi wao haikutofautiana na
wajinga.
Hata hapa nchini kuna baadhi ya viongozi serikalini,
kwenye mashirika na hata kwenye sekta binafsi ambao wakikuonesha vyeti
vyao vya shule unaweza kuogopa, lakini utendaji wao ni kichefuchefu.
Kisaikolijia
sifa za kiongozi ziko wazi na ni muhimu, mtu kuwa nazo kabla au baada
ya kupewa cheo. Leo tunataka kuziangalia kwa undani sifa hizi, ili kama
wananchi au viongozi wenye dhamana ya kuchagua watu wa kuongoza
tuwatazame watu kwa sifa zao kabla na baada ya kuwapa nafasi. Sifa za
kiongozi ni hizi zifuatazo:
Awaze mafanikio makubwa
Kiongozi
bora lazima awe na maono ya juu ya kuhakikisha kuwa nchi yake, kampuni
yake sekta yake inapata mafanikio makubwa, hii ndiyo itakuwa dira ya
kazi yake itakayompa muongozo wa kusimamia wafanyakazi na watendaji wote
walio chini yake kufikia kiwango cha mafanikio anachokiwaza. Kiongozi
asiyekuwa na mawazo ya juu ya kuendelea kutoka mahali alipo hafai.
Awe na nia
Haitoshi
kwa kiongozi kuwa na mawazo chanya peke yake bila kuwa na nia ya
kuyatimiza. Hivyo, kiongozi atafaa kuchaguliwa kuwa kiongozi endapo tu
atakuwa na uwezo wa kuratibu vema na kutekeleza alichowaza. Ajue njia
anayopita, awatangulie anaowaongoza kwa vitendo.
Ajitambue mwenyewe
Lazima
kiongozi ajitambue mwenyewe ni mtu wa namna gani, ajue uwezo wake na
upungufu wake na awe tayari kujiongezea maarifa kila siku, ili aweze
kukabili changamoto na mabadiliko ya ulimwengu. Asome, afuatilie mambo
yanavyokwenda na ajifunze kwa wenzake kuhusu kufanikisha malengo yake.
Asimamie maamuzi
Kuna
wakati malengo hukumbana na vikwazo, hivyo ni wajibu wa kiongozi
kusimamia maamuzi sahihi na kuwa mtu wa mwisho. Kiongozi mwenye
kubadilika badilika kama kinyonga, hafai kwa vile kukosa msimamo kuna
maanisha udhaifu wa mipango na kujiamini.
Adhibiti msongo wa mawazo
Tunamtarajia
kiongozi mzuri awe ni mtu mwenye kupunguza msongo wa mawazo, ili
kuifanya akili yake ifikie maamuzi sahihi, lakini kama atakuwa mwenye
kuwaza mengi, atajikuta anachanganyikiwa na kuwa mtu wa jazba katika
maamuzi na hivyo kuipotosha jamii.
Akubali kukosolewa
Viongozi
wasiokuwa na sifa za uongozi huwa hawakubali kukosolewa, wakidhani kuwa
hiyo ndiyo njia ya kuthibitisha msimamo wao na usahihi wao. Kiongozi
makini ni yule ambaye atakuwa tayari kukosolewa na kuwapongeza
wanaomkosoa kwa kutazama mwenendo wake na usahihi wake. Asiyekubali
kukosolewa hafai kuwa kiongozi.
Awe msikilizaji
Kiongozi
mzuri ni yule ambaye atakuwa tayari kuwasilikiza watu walio chini yake,
apokee maoni yao na ikiwezekana ayafanyie kazi. Lakini pia anatakiwa
kuwafahamu kwa undani, ili aweze kuwaongoza vema kufuatana na hali zao.
Akiwa na watu walemavu wenye kasoro kadhaa wa kadhaa anatakiwa
kuwatambua kabla na baada ya kuwa kiongozi wao. Kuongoza usichokifahamu
ni ujinga.
Afuate haki
Kiongozi imara anatakiwa kufuata
haki katika kuongoza kwake, asijione mwenye haki zaidi ya wale
anaowaongoza katika sheria. Ni muhimu kwake kuwafanya walio chini yake
kujiona wako huru katika mawazo na matendo. Kiongozi anayetumia nguvu na
ukali kuongoza watu hafai. Hata yule mwenye kujivunia uongozi wake naye
hafai.
Awe egemeo la watu
Sifa nyingine ya kiongozi ni kuwa
egemeo la watu wake katika shida na raha. Kiongozi mzuri ni yule ambaye
atakuwa tayari kusikitika, kuomboleza, kufurahi pamoja na watu wa chini
yake bila kujitenga nao. Ajitolee kuwatumikia watu kwa hali na mali na
awe tayari kutumika zaidi kwa maslahi ya wengine.
Atie moyo watu
Kiongozi
mzuri ni yule ambaye atakuwa na uwezo wa kuwatia moyo walio chini yake
ili waweze kuendeleza vipaji vyao. Haipendezi kwa kiongozi kuwavunja
moyo watu kwa kauli za kudharau kazi na jitihada zao walizojaribu
kufanya katika kutekeleza majukumu yao kama wafanyakazi au wananchi.
Afurahie mafanikio
Sifa
nyingine muhimu ya kiongozi ni kuwa tayari kufurahia mafanikio
aliyopata pamoja na watu wake. Ni wajibu wa kiongozi kutoa tuzo,
kuwashukuru wafanyakazi wake na kuwa tayari kuwapa ofa. Hii itasaidia
kuwafanya watu waone hawajapoteza nguvu zao katika utendaji wao na
kwamba wanakubalika. Si busara wakati mwingine kuwakosoa watu mbele ya
hadhara na kueleza kutofurahishwa na kazi zao.
Aungane na wa chini yake
Mtu
kuwa kiongozi haimaanishi amekuwa wa tofauti na watu wengine kiasi cha
kushindwa kuchangamana nao kama wanavyofanya baadhi ya viongozi.
Kiongozi mwema ni yule atakayeungana na watu wake katika maisha ya
kawaida. Kuwa kiongozi haimaanishi kwamba watu watakufuata wewe kila
siku, wakati mwingine wewe unatakiwa kuwafuata wao na kuwa nyuma yao
hata mahali walipokosea au wanapokabiliwa na makosa, watetee na uoneshe
kuwajali na kuwapigania, makosa utayahesabu baada ya utetezi wako
kukamilika.
Akubali lawama
Kama kiongozi amefanya
mambo ambayo jamii haikupendezwa nayo anachotakiwa kufanya ni kukubali
kulaumiwa. Ikiwa anaongoza kitego cha umeme kwa mfano na watu hawakupata
nishati hiyo kwa wakati hatakiwi kukwepa lawama, vivyo hivyo kwenye
wizara na idara au nchi kwa ujumla.
Afahamu kutatua matatizo
Kiongozi
mzuri ni yule ambaye atakuwa na uwezo wa kuzuia migogoro na kuitatua
kwa haraka. Muongozo mzuri katika eneo hili umesimama katika mawasiliano
na watu wa chini, mawasiliano haya ndiyo yatakayomuwezesha kiongozi
kujua matatizo waliyonayo wafanyakazi wake au hata jamii anayoiongoza na
hivyo kumfanya apate wasaa wa kuyashughulikia mapema.
Ajifunze kwa makosa
Wakati
mwingine mawazo na mipango inaweza ikaenda kombo, hivyo ni wajibu wa
kiongozi kujifunza kutokana na makosa yake au ya wale anaowaongoza, ili
kuepuka kurudia makosa yale yale na kumfanya apoteze sifa za kuwa
kiongozi mzuri.
Mwanafalsafa Winston Churchill aliwahi kusema "The price of greatness is responsibility." Thamani ya ukuu ni uwajibikaji.
Awe mwaminifu
Miongoni
mwa maeneo magumu kabisa yaliyowashinda na yanayoendelea kuwashinda
viongozi wengi ni uaminifu. Kiongozi bora ni yule ambaye yuko tayari
kusimamia muongozo wa katiba ya nchi au marufuku alizowekewa katika
madaraka yake. Hii inakwenda sambamba na kutowaonea, kuwanyanyasa wa
nchini yake kwa kutumia cheo chake.
Awe mkweli
Viongozi wengi
hasa wa kisiasa siku hizi ni waongo hakuna mfano, wamejaa ahadi
zisizotekelezeka na hata wanapogundua kuwa hawana uwezo au wamekwama
kuzitimiza, hawaoni haja ya kutubu mbele ya wanaowaongoza. Kiongozi
makini ni yule atayekuwa tayari kuonesha ubora wa matendo na kauli zake.
Asiwe mwenye majungu
Kuna
baadhi ya viongozi kwenye maofisi wanaendekeza sana majungu na pengine
kuyapa umuhimu wa hali ya juu. Hii ni sifa mbaya kwa kiongozi yo yote,
hivyo anayetumikia ‘umbea’ katika ofisi aliyokabidhiwa kama mkuu
anapaswa kuondolewa. Kiongozi makini atatumia uwezo wake kuzuia watu
wasimsengenye/wasisengenyane kwa kuwa muwazi na mwenye kufungua milango
ya watu kumuona na kumlaumu na kueleza hisia zao.
Awe bora
Kwa
kila analofanya kama kiongozi lazima alifanye kwa ubora, asiwe mtu
mwenye kulipua kazi na kufanya chini ya kiwango cha uwezo wake. Kila
siku katika kazi, maamuzi, usimamizi, utekelezaji lazima atumike zaidi
ya uwezo wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni