21.7.14

NGUVU YA MTOTO WA NJE YA NDOA

 Wanyakyusa huwa tunaita (Nsighwana) yaani mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa. Huyu mtoto ana nguvu sana katika ulimwengu wa roho na mpaka kwenye ulimwengu wa kimwili, na hizo nguvu zimegawanyika kwenye maeneo mawili:
1)      Eneo la Kwanza, huyu mtoto huwa anafanyika kama lango la baraka.
Haijalishi anaishi mazingira gani, au anaishi na walezi ambao siyo mama yake wa kumzaa au baba yake wa kumzaa, pengine anaishi na bibi yake au amepanga. Lakini muda mwingine huyu mtoto, Mungu huwa anamtumia kama lango la baraka.
“Basi huyo Yefta, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yefta. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekuwa wakubwa wakamtoa Yefta, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine. Ndipo Yefta akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu;……….wakaenda kumtwaa huyo Yefta katika ile nchi ya Tobu; wakamwambia Yefta, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni”
(Waamuzi 11:1,3;5,6)
Huyu Yefta, alikuwa ni mtoto wa nje ya ndoa lakini Mungu aliachilia nguvu zake na baraka juu yake kwa ajili ya familia yake na kwa taifa zima la Israeli. Nimeona watoto, vijana wengi wanakuwa na akili sana darasani lakini ukifuatilia vizuri mmoja wapo, kuishi kwake na wazazi wake, utashangaa akikwambia anaishi na mama tu! kwani alitelekezwa na baba, na kwenda kuoa mwanamke mwingine. Wengine wanamaisha mazuri, Mungu kawabariki lakini baba alimkataa, na huko baba yake aliko maisha yake yanakuwa siyo mazuri sana. Ni wakina baba wangapi wamezaa nje ya ndoa na wamewakataa hao watoto, na maisha yao hao wazazi yakoje? Kama siyo mlevi basi atakuwa ni Malaya, ama mwizi. Mara nyingi kufanikiwa kwa hao watu ni vigumu sana, au anaweza kufanikiwa lakini nje ya njia za Mungu, kitu tunachosema ni mafanikio feki na yasiyokuwa na uzima wa milele ndani yake.
      Unamkumbuka Sulemani? Fuatilia kuzaliwa kwake ilivyokuwa. 2Samweli 12,13 (soma sura hizo). Utaona mfamle Daudi alipokuwa akitembea juua ya dari ya jumba lake la kifalme, ghafula akamwona mwanamke akioga na huyo mwanamke alikuwa anaitwa Bath-sheba, na alikuwa ni mke wa Uria aliyekuwa ni askari wa mfalme Daudi. Mfalme Daudi akafanya namna alivyofanya akampata yule mwanamke, akazini naye na yule mwanamke akapata mimba. Mtoto alipozaliwa, Mungu akamuua yule mtoto ingawa Daudi alifunga siku saba na kuomba sana. Lakini yale maombi yalikuwa yanazaa tunda ambalo Mungu alilikusudia.
v  Mungu alikuwa anamwondolea aibu mfalme Daudi kwa watu kupitia yule mtoto, endapo angeishi. Ndiyo maana mtoto alipofariki tu, Daudi akainuka na akaacha kuomba juu ya huyo mtoto.
v  Kupitia yale maombi, Mungu alikuwa anaumba mtoto mwingine atakaye mpenda, ambaye alikuja kuwa Suleimani, aliyezaliwa kupitia tumbo la huyo Bath-sheba. Ndiyo maana hata Adamu ilimgharimu sana kwa muda kuja kumzaa Sethi, ambaye atakubalika na Mungu.
Nilikuwa namuuliza Mungu, kwanini hakutokea mtoto uliyempenda kutoka kwa mfalme Daudi, aliyezaliwa mbali na tumbo la Bath-sheba? Nisikilize mzazi itakusaidia sana! Mfalme Daudi alipokuwa anazini na Bath-sheba, ujue kwamba alikuwa na wake wengine nyumbani kwake. kilichomfanya aende nje ya ndoa ni nini? Maandiko yanasema “naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho”. Inaonekana Daudi wake zake hakuwapenda kwa dhati kama huyu Bath-sheba. Mungu aliachlia mbegu iliyobora kwenye tumbo la Bath-sheba kutoka kwa Daudi kwani ulikuwepo upendo wa dhati. Unapompenda mke wako kwa dhati, ujue hata utakachokizaa kitapendwa na Mungu kwani Mungu mwenyewe ni pendo (1Yohana 4:8), hivyo unapoingia kwenye ile ibada na mkeo/mumeo msipokuwa na upendo wa dhati au mmekorofishana, au mnaingia ile basi tu! Nawaambieni mtazaa mtoto mwenye hasira, muda mwingine utashangaa anazaliwa mtoto kilema, kwa sababu mlimtafuta huyo mtoto mkiwa hamna amani wala hamkupendana kwa dhati.
    Sulemani alikuja kutumika kama mlango wa baraka ndani ya familia ya Daudi, kwani ndiye aliyekuja kukubaliwa na Mungu akae kwenye kiti cha ufalme alipotoka baba yake Daudi. Lakini kuzaliwa kwake kulikuwa ni kwa hali ambayo haikuwa halali, kwani alikuwa amezaliwa nje ya ndoa ambayo Mungu alikuwa amempatia mfalme Daudi. Fuatilia watu ambao ni viongozi mahali mbali mbali, utaona kwamba wengine walilelewa na mama tu, kwani baba alimkataa.
     Usije ukajaribu wewe mama kumtupa mtoto uliyezalishwa nje ya ndoa hata kama amekutelekeza huyo mwanamume aliyekupa ujauzito. Kumbuka Hajiri:
“Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa”
(Mwanzo 21:16,18)
Nataka uone neno hili “…Mungu akasikia sauti ya kijana..” kwa nini Mungu hakusikia sauti ya Hajiri? Mungu anapokupa mtoto kwenye wakati mgumu, haijalishi umekataliwa au la! Lakini ujue kwamba Mungu anakuwa na makusudi na huyo mtoto, la sivyo angeamua kumuua mapema, kama mtoto wa Daudi. Maisha ya baraka na mafanikio ya wazazi yanafichwa ndani ya mtoto na ndiyo maana Mungu alisikia kilio cha kijana (mtoto) ambaye alikuwa ni Ishimaili. Umewahi kufikiria, ingekuwaje endapo Hajiri angeamua kutokwenda kumchukua mwanae! Ni wasichana wangapi wametupa watoto, wametoa mimba, na wamekwama kimaisha na kiroho kwani Mungu alikuwa ameachilia baraka zao kupitia wale watoto waliowatupa.
      Wazazi huwa wanaelewa, mara nyingi inapotokea mtu kajifungua, huwa wanaelewa kuwa huyu mtoto amekuja na baraka fulani. Utashangaa wageni wanakuwa wengi nyumbani, chakula hakiishi ndani, na kadhalika. Wengine wanasema mtoto mchanga huwa anawaombea wazazi kwa Mungu kwani ni malaika, ni kweli kabisa. Mungu atamsikiliza mtoto kuliko mama au baba, na ndiyo maana Mungu alisikia kilio cha Ishamaili na siyo cha Hajiri.
       Kama ulizaa nje ya ndoa, na mtoto huyo yupo, nakushauri ukamchukue na kama hukumwambia mkeo au mumeo, ni wakati wa kumwomba Mungu akupe ujasiri na hekima ya kusema naye ili akuelewe na usivunje ndoa yako. Utashangaa umekwama kiuchumi, kumbe kuna damu inakulilia huko nje. Na uwe na uhakika huyo mtoto Mungu atakuja kumfanikisha tu, hata kama hutamchukua, na baadaye utajutia kwanini hukuwa muwazi. Unakataa mtoto, tambua unakataa baraka za Mungu.

MWENDELEZO WA SOMO

2)      Usipojua namna ya kumkabidhi Mungu, huyu mtoto anafanyika kuwa laana kwenye ndoa. 
“Gidion alikuwa na wana sabini waliozawa na mwili wake; kwa maana alikuwa na wake wengi. Na suria yake aliyekuwako Shekemu, yeye naye alimzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki.”
(Waamuzi 8:30-31)
“Kisha akaenda (Abimeleki) nyumbani kwa babaye huko Ofra, akawaua nduguze, hao wana wa Yerubaali, watu sabini akawaua juu ya jiwe moja;…”
(Waamuzi 9:5)
Abimeleki alizaliwa na Suria (Girl friend) wa Gidion, inamaana alizaliwa nje ya ndoa, lakini amekuwa mwiba kwa uzao wote wa Gidion ambao walikuwa ndani ya ndoa. Akapelekea kuwaua nduguze, watoto wa babaye Gidion.
             Nimeona ndoa nyingi sana zinavunjika kwa sababu ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa. Zingine ni ndoa za wapendwa (waliookoka) lakini kwa kutokujua, walijikuta wakati wa ujana wao walicheza na dunia mwishowe wakazaa na watoto. Nataka ujue sababu hasa, kwanini watoto wa nje ya ndoa, wanapoingia kwenye mazingira ya ndoa halisi huwa wanasababisha migogoro ndani ya ndoa. Haijalishi amebadilika ukubwani, lakini kwanini ilete kutokuelewana kwa wanandoa na familia nzima, mara nyingine inapelekea ukoo mzima kutokuelewana na huyo muhusika (aliyezalisha).
v     Tambua yule mtoto alizaliwa chini ya agano.
“Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya BWANA kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia. Lakini ninyi mwasema, ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtendea mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako”
(Malaki 2:13,14)
Agano ni makubaliano, mkataba, kiapo baina ya pande mbili au watu wawili. Sasa agano ambalo linanguvu zaidi ni agano la damu, na kama ilipelekea mpaka kuzaa mtoto na huyo msichana, ina maana agano lililotendeka hapo ni agano la damu. Kama mlifanya uasherati inamana Mungu hakuwepo kwenye hilo agano, inamaana Shetani ndiye aliyehusika, maana hakuwa mke wako halali mbele za Mungu. Pindi unapomwacha uwe na uhakika lile agano linaendelea kukutafuta wewe uliyefunga na huyo msichana/mwanamume.
      Agano likitendeka la damu, mara nyingi huwa linakuwa linahitaji damu nyingine, na ndiyo mana kama imetokea ajali mahali fulani na ikaua watu, utashangaa ajali nyingine inatokea, kwani kuna mapepo yanayoendelea kufwatilia damu nyingine mahali pale. Hivyo anapotokea mtoto uliyemzaa nje ya ndoa, inamana anakuja na roho ya lile agano, likikutaka uende tena kufunga agano lingine, yaani ukaendelee kuzini, ndiyo maana inatokea hali ya kumchukia mke wako na kwenda nje ya ndoa tena, pasipo mwenyewe kujua.
v     Roho ya uasherati inakuwa inafwatilia kulipiza kisasi.
Baada ya kumwagika damu ya Habili, maandiko yanasema “….sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka kwenye ardhi” (Mwanzo 4:10b). damu ya Habili ilikuwa inalia ili kulipiza kisasi kwa Kaini. Hiyo damu inapokuja na kutaka kulipiza kisasi ndani ya nyumba, inakuwa inamuhitaji mtu aliye dhaifu kati yenu ninyi wana ndoa, ili aende kinyume na kiapo (agano) walichokifunga pale walipokuwa wanafunga ndoa. Utashangaa sana mke wa mtu anaamua kutoka nje ya ndoa na kuzini ilimradi amkomoe mume wake, kwani amemwona akiwa na wengine huko, na aliwahi kuzaa nje ya ndoa. Kitendo cha mwanamke kutoka nje ya ndoa, tayari hiyo ni roho ya kisasi inayotokana na agano alilolitenda mume wake, kwa kuzaa nje ya ndoa.
“BWANA asema hivi, Angalia nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili”
(2Samweli 12:11)
“Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote”
(2Samweli 16:22)
Ni habari za mfalme Daudi, baada ya kutembea na Bath-sheba na kumpa mimba, ingawa mtoto alikufa baada ya siku saba, na alikuwa ni mke wa mtu (Uria) aliyekuwa ni askari wake Daudi. Yaani Daudi katembea na mke wa mtumishi wake, na akasababisha mimba, na Mungu akamwambia Daudi kwamba na yeye atafanyiwa kama vile vile alivyomfanyia mtumishi wake, tena pasipo siri.
v     Inafuatilia watoto.
Kumbuka Absalomu alikuwa mtoto wa Daudi, na ndiye aliyetembea na masuria wa baba yake, na si mtu mwingine! (1Samweli 16:22). Chunguza, kama baba aliwahi kuzaa nje ya ndoa, utashangaa mtoto pia anakuja kuzaa nje ya ndoa. Kama baba anazini na watoto wa marafiki zako, uwe na uhakika, watoto wake watapewa mimba na rafiki zake hao hao. Haya mambo yapo kwenye jamii tunazoishi nazo sisi wenyewe na siyo kuzimu! Ndiyo maana kila siku kizazi kinaendelea kuharibika, na kufikia mpaka miaka ya kuishi inapungua (life expand). Mtoto wa miaka kumi na mbili anazaa mtoto, yaani mtoto anazaa mtoto.
v     Inakuja na roho ya mauti.
Kuna habari nilisikia mkoa fulani, baba wa kambo alimuua mtoto kikatili sana, kwa wivu aliokuwa nao. Alimwoa mwanamke ambaye alikuwa ameshazalishwa na mtu mwingine, lakini kumbe ndani yake yule mwanamume alikuwa anamchukia yule mtoto, hatimaye ikapelekea kifo na yeye akaishia jela. Mungu atusaidie wazazi!
v     Inafunga milango ya baraka na mafanikio.
Kunakitu ndani ya familia yako lazima kitakwama tu! Mfano, utakuta familia zingine ni ngumu kupata watoto kiurahisi, kama kuna mifugo, utashangaa inaanza kudhoofika mpaka kufa, chuki kwa mke/mume wako pasipo sababu, kama unawatoto wengine, utashangaa wanabadilika akili darasani (kushuka kwa ufahamu). Mpaka unakuja kufikia wakati mtakapogundua kwamba chanzo ni huyo mtoto wa nje ya ndoa, mtaanza kusema ni mchawi na kumbe siyo mchawi bali ni roho iliyo ndani yake ambayo hata yeye anashindwa kuitambua.

Ø      Utaepukaje kama uliisha zaa nje ya ndoa? Kaa vizuri na Mungu, uvunje hiyo roho ya uasherati.
“Basi mtiini Mungu, Mpingeni Shetani naye atawakimbia”
(Yakobo 4:7)
Kumbuka kuomba toba juu yako, juu ya mwanamke uliyemzalisha, juu ya mtoto husika, pamoja na familia yako. Kuna dada mmoja, nilikuwa namfanyia maombi na shida yake kubwa ilikuwa ni ndoa haina amani, ghafla Roho Mtakatifu akaniambia juu ya mume wake kwamba ana mtoto nje ya ndoa. Naye akakiri kwamba ni kweli na amewahi kumshirikisha kwamba yupo kwa ndugu zake. Na mume wake alikuwa hatulii nyumbani, na alikuwa ana wanawake wa nje wengi sana, lakini kumbe chanzo cha magomvi yote ni yule mtoto. Tulipoingia kwenye maombi, Mungu akanipa maelekezo ya kumrudisha mtoto nyumbani ili akae na yule dada iwe familia moja.
        Unapomleta nyumbani kama familia moja, unakuwa unavunja nguvu ya ile roho ya uasherati, isiwe na nguvu, ila hakikisha umekaa vizuri na Mungu, maana utajikuta unaongeza tatizo badala ya kuondoa tatizo. Ashukuriwe Yesu Kristo yule mama akarudisha mahusiano mazuri kwa mume wake na familia nzima.
Ø      Vunja hilo agano kwa njia ya sadaka.

Kama agano lilitengenezwa kwa damu, ambayo damu ilikuwa inahusika kwenye utoaji wa sadaka. Hivyo chukua sadaka na maombi yako, nenda ukavunje hilo agano madhabahuni pa BWANA, na Mungu atasimama kwenye hilo eneo daima. Mungu alisema na huyo dada aliyekuwa anashida ya ndoa, iliyosababishwa na mtoto wa nje ya ndoa kwamba atoe sadaka. Alipotoa sadaka na nilipoanza kuiombea, ghafula nguvu za Mungu zilishuka na kumwangusha chini. Mara pepo likaanza kupiga kelele na kulalamika kwanini ametoa sadaka, kwani pepo linasema lilifunga agano na mume wake, na hilo agano ndilo lile la mtoto wa nje ya ndoa pamoja na wanawake aliokuwa akizini nao. Nakumbuka ulikuwa ugomvi mkubwa sana na ashukuriwe Yesu Kristo sadaka haikurudishwa na akafunguliwa, na ndoa yake ikaponywa.

Barikiwa sana, kwa msaada zaidi
ingia kurasa ya mawasiliano.

Maoni 1 :

  1. Mpenzi wangu aliachana na mimi, najua ilikuwa kosa langu ambalo lilimfanya aachane na mimi, akanipata nikiongea juu yake, kuna kijana niliyemwita rafiki yangu alinivuta na kufanya naye mapenzi kisha mpenzi wangu akatushika, basi aliachana na mimi, ninampenda sana, nilifurahisha kwa wiki na miezi hakukubali kunikubali, nilikuwa nikisoma mkondoni jinsi ya kumrudisha mpenzi wangu basi nilikuta na makala juu ya jinsi mwanamke alirudi Mumewe aliyempa talaka, alisema kuwa Dk Lomi amsaidia alifanya sala kadhaa na mumewe amerejea kwake, basi na mimi nikawasiliana na Dr Lomi na kuelezea kile kilichotokea kisha akanisaidia kufanya maombi kadhaa na mpenzi wangu akarudi akiniombea alijuta kuwa bado ananipenda na leo tumerudi pamoja na naahidi kamwe hatutazungumza juu yake na leo tunafurahi, ikiwa unahitaji pia Msaidizi wa Dk Lomi kuwasiliana naye kwenye Line ya nambari ya WhatsApp; +2349034287285 unaweza pia kumtumia barua pepe; lomiultimatetemple@gmail.com kwa msaada

    JibuFuta